Serikali yazungumza kupata mikopo ya kibiashara ya trilioni 2.1/-

SERIKALI inafanya mazungumzo na taasisi za kifedha ambazo zinakopesha ili iweze kuikopesha kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17.

Hali hiyo inatokana na kuwepo kwa masharti magumu yanayowekwa na taasisi za kifedha za nje pamoja na nchi wahisani ambazo zimekuwa zinaikopesha serikali katika kutekeleza bajeti yake yake katika miezi mitano ya kuanza kutumika kwa bajeti ya mwaka huu wa fedha.

Pia Serikali imesema kwamba ina matumaini kwamba hivi karibuni itakamilisha mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa lengo la kupata mkopo wenye masharti nafuu.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya uchumi wa nchi.

“Serikali ilitarajia kukopa mikopo ya kibiashara ya Sh trilioni 2.1 kutoka kwa taasisi mbalimbali za kifedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali, lakini kutokana na masharti magumu ikiwemo riba kubwa hatukuweza kufanya hivyo,” alisema.

Dk Mpango aliongeza kuwa kwa sasa Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, Kuwait, Abu Dhabi na Jumuiya ya nchi zinazouza mafuta kwa wingi (Opec).

Kwa mujibu wa waziri huyo, gharama kubwa za kukopa zimechangiwa na hali ya uchumi wa nchi za Ulaya kuyumba na hivyo kusababisha kuongezeka kwa riba kiati ya asilimia 9 na sita kwa mwaka.

Kutokana na hali hiyo Serikali imeahirisha kuomba mikopo katika nchi hizo na badala yake imeelekeza nguvu katika nchi za China, India, Korea Kusini na Japan. Pia alisema wanafanya mazungumzo na Suissuie Bank ya Uingereza ili wakope dola za Marekani milioni 300 .