Bei ya petroli yapanda, dizeli yashuka

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta nchi nzima, ambazo zimeanza kutumika jana.

Ewura imesema bei za rejareja za dizeli na mafuta ya taa, zimepungua huku petroli imepanda.

Aidha imesema pia kuwa hakutakuwa na mabadiliko ya bei za mafuta kwa mkoa wa Tanga, kutokana na kutopokewa mzigo mpya wa mafuta kwenye bandari ya mkoa huo kwa mwezi wa Desemba mwaka jana.

“Kwa Januari 2017, bei za rejareja kwa dizeli na mafuta ya taa zimepungua kwa Sh 66 sawa na asilimia 3.68 na Sh 37 sawa na asilimia 2.11, na kwa mafuta ya petroli bei imeongezeka kidogo kwa Sh 0.10 kwa lita sawa na asilimia 0.01,” alisema Mkurugenzi Mkuu Ewura, Felix Nyamlagosi katika tangazo alilolitoa kwa umma kupitia vyombo vya habari jana.

Ngamlagosi alisema bei za rejareja kwa mafuta ya aina zote yaani petroli, dizeli na mafuta ya taa zimebadilika, ikilinganishwa zilizotolewa Desemba 7 mwaka jana. Katika taarifa hiyo, Nyamlagosi alisema mabadiliko hayo yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia.

Kwa Dare s Salaam sasa petroli itauzwa kwa Sh 1890, dizeli Sh 1732 na mafuta ya taa Sh 1700 kwa lita.

Mwezi uliopita, bei za jumla kwa mafuta ya dizeli na mafuta ya taa, nazo zilipungua kwa Sh 66 sawa na asilimia 3.91 na Sh 37 sawa na asilimia 2.25 kwa lita na kwa petroli bei iiliongezeka kidogo kwa Sh 0.01 sawa na asilimia 0.01.