Serikali yasema hakuna mdororo wa uchumi

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango amesema hakuna mdororo wa uchumi nchini.

Akitoa kauli ya serikali bungeni kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi wa taifa mjini Dodoma jana, aliwahakikishia wabunge kwamba hakuna mdororo wa uchumi nchini.

Alisema viashiria mbalimbali vya kiuchumi, ikiwamo ukuaji wa uchumi, mfumko wa bei, mwenendo wa sekta ya nje na akiba ya fedha za kigeni, mwenendo wa sekta ya fedha, ikiwa ni pamoja na haki ya ukwasi na deni la Taifa, vinaonesha uchumi wa Tanzania, upo imara na tulivu.

Dk Mpango alisema takwimu za ukuaji wa Pato la Taifa zinaonesha kwamba uchumi wa taifa unaendelea kukua na Tanzania imebaki kuwa miongoni mwa nchi za Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambayo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi.

Alieleza kuwa ukuaji wa Pato la Taifa katika mwaka 2006, ulitarajiwa kuwa asilimia 7.2, lakini tathmini iliyofanywa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inaonesha ukuaji wa uchumi utakuwa wa wastani wa asilimia 7.0, ambayo ni kubwa zaidi kuliko nchi nyingine Afrika Mashariki.

Kuhusu benki, Dk Mpango alisema bado zina ukwasi wa kutosha wa kuweza kukopesha wananchi. Akiba za fedha za kigeni Desemba 2016, akiba ya fedha hizo ilifikia dola za Marekani milioni 4,325.6 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutioka nje kwa miezi 4.2.

Kuhusu deni la taifa, alisema linaendelea kuwa ni himilivu, tathmini, kufikia Desemba, 2016, likijumuisha deni la ndani na la nje, lilifikia Dola za Marekani milioni 19,021.9 ikilinganisha nwa dola milioni 18,459.3 Juni, 2016 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 3.05.