Wanaolazimisha malipo kwa fedha za kigeni waonywa

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amekataza mtindo wa kukataa malipo kwa shilingi na kutaka kulipwa kwa fedha za kigeni ikiwamo dola ya Marekani.

Waziri alikuwa akijibu swali la nyongeza la Jaku Hashimu Ayoub (CCM) aliyelalamika kwamba kuna vyuo nchini ambavyo vinatoza ada wanafunzi kwa kutumia dola za Marekani badala ya shilingi.

Waziri Mpango alisema sheria ya usimamizi wa fedha ya mwaka 1992 inaruhusu mtu kupokea, kumiliki fedha kwa shughuli za kiuchumi. Sheria ya Benki Kuu(BoT) ya 2006, shilingi ya Tanzania ni fedha halali katika kulipia ada lakini haikatazwi kuonesha malipo hayo kwa kutumia dola, lakini ni kosa kukataza kulipa kwa kutumia shilingi.

Mpango alisema utafiti uliofanywa na BoT umeonesha kwamba ni asilimia tatu tu ya shughuli za kuuchumi nchini zinazotumia dola, lakini ni kosa kukataa kutumia shilingi.

Akijibu swali la msingi la mbunge huyo kuhusu malipo ya ada kwa dola, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya ufundi, Stella Manyanya alisema, hakuna sheria yoyote inayotumika kwa mwanachuo kulipa ada kwa fedha za kigeni.

Alisema sarafu inayotumika nchini ni shilingi ya kitanzania kwa mujibu wa kifungu 25 na 26 cha sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, hivyo malipo yoyote yanatakiwa kufanyika kwa fedha hiyo kama ilivyoainishwa katika kufungu cha 28 ya sheria hiyo.