TCRA:Kuhama kampuni ya simu si lazima

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeeleza kuwa, wateja wa huduma za simu za mkononi nchini hawapaswi kulazimishwa kuhama kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine, kwani jambo hilo ni la hiyari.

Mamlaka hiyo imetoa maelezo hayo zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa huduma ya kuhama kutoka mtandao mmoja wa simu kwenda mwingine bila kubadili namba inayotarajiwa kuanza Machi Mosi, mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa elimu kwa umma kuhusu huduma ya kuhama kutoka mtandao mmoja wa simu kwenda mtandao mwingine bila kubadilisha namba, akisema huduma hiyo ni ya hiari na si lazima.

Alisema huduma hiyo ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa Kanuni za Mwaka 2011 za Sheria ya Mawasiliano ambapo mhamaji ataondolewa usumbufu wa kulazimika kuwataarifu watu wake na kumpa uhuru mtumiaji kuchagua mtoa huduma anayemtaka.

“Huu ni utaratibu wa hiari kwa sababu hii ni fursa ya mawasiliano kama fursa nyingine ambazo zimeanzishwa za kutuma na kupokea fedha, hivyo wananchi hawatakiwi kulazimishwa kuhama au kuzuiliwa kuhama,” alisema.

Kilaba alisema huduma hiyo pia itaongeza ushindani kwenye sekta ya mawasiliano na hivyo kuwa kichocheo cha utoaji huduma bora.

“Mfumo huu wa kuhamia mtandao mwingine utatumiwa na wateja wote wanaolipia huduma kwanza na wale wanaolipia huduma baada ya matumizi, na ili kuingia kwenye mfumo huu, simu ya mtumiaji lazima iwe inatumika yaani haijafungiwa au kusimamishwa kwa muda,” alisema.

Akizungumzia utaratibu wa kuhama, Mhandisi wa Mawasiliano TCRA, Mwesigwa Felician, alisema mteja atabaki na namba yake ya awali kutoka mtoa huduma mmoja kwenye mwingine na kuwa mteja atapokea simu na ujumbe mfupi wa maneno bila kujali ni mtandao upi amehamia bila kuwataarifu watu wake.

Alisema pia mteja hawezi kuhama na salio lililopo, na anatakiwa kutumia salio kabla ya kuhamia kwingine vinginevyo salio litapotea na pia hawezi kuhama kama ana mkopo na kama namba inahusishwa na uhalifu.

Alisema mtumiaji anayetaka kuhama anatakiwa kwenda vituo vya mauzo au wakala anayetambulika na kujaza fomu maalumu ambayo inachukuliwa kama tamko rasmi na kutakiwa kutoa vitambulisho.

“Ukishajaza fomu utatakiwa kutuma meseji yenye neno HAMA kwenda namba 15080 ambayo ni namba maalumu ya kuhama na hapo utajulishwa kama maombi yako yamepokelewa. Endapo namba yako haijazuiliwa kutokana na sababu mbalimbali basi utajulishwa kwa meseji,” alisema.

Huduma hiyo katika Afrika imeanzishwa katika nchi za Misri, Kenya, Sudan, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Senegal na Morocco wakati nchi za Rwanda na Namibia zipo mbioni kuanzisha.