Kituo cha forodha Tanzania, Zambia chaanza kutumika

KITUO cha Pamoja cha Forodha cha mpaka kati ya Tanzania na Zambia (Tunduma/Nakonde) kimeanza rasmi kutumika licha ya kukabiliwa na msongamano mkubwa wa magari unaotakiwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Kituo hicho kimeanza kufanya kazi tangu Februari mosi mwaka huu, ambako watumiaji wa mpaka huo watakuwa wakihudumiwa upande mmoja wa mpaka, badala ya utaratibu uliokuwa ukitumika awali ambapo watumiaji walilazimika kukaguliwa mizigo yao kila upande hatua iliyokuwa ikichelewesha biashara katika mpaka huo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamis Shaaban, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, wameeleza kuridhishwa na kazi inayofanyika mpakani hapo kupitia mfumo huo mpya.

Hata hivyo, baadhi ya madereva wanaosafirisha bidhaa kupitia mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, pamoja na kupongeza utaratibu huo mpya, wameiomba serikali iwasiliane na upande wa Zambia, ili waongeze kasi ya kuruhusu malori kuendelea na safari yanapofika mpakani hapo bila kucheleweshwa ili kwenda sambamba na kasi ya upande wa Tanzania, ambao umeboresha kwa kiwango kikubwa utoaji wa huduma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Mkenda alisema makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na watoa huduma katika mpaka huo yalikuwa ni kuwahudumia wadau wanaotumia mpaka huo kwa muda usiozidi siku moja na kuwataka madereva wa malori wanaokwazwa kuwasiliana na mamlaka zinazohusika.

Profesa Mkenda amewaonya mawakala wa forodha katika mipaka yote nchini watakaobainika kwa namna moja au nyingine kuwachelewesha wenye malori kwa makusudi watafutiwa leseni zao za kufanya biashara hiyo.

Alisema serikali imeunda timu ya wataalamu wanaopitia kero mbalimbali za mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini, itakayopeleka mapendekezo namna ya kuboresha mazingira hayo kwa kuwa mchango wa sekta binafsi wakiwemo wawekezaji, unatambuliwa na serikali.

Ofisa Mfawidhi wa Forodha, Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa-Tunduma, Magori Magori, na Mbunge wa Jimbo la Tunduma, Frank Mwakajoka, walielezea kukithiri kwa vitendo vya magendo mpakani na kero ya vizuizi lukuki kwenye njia kuu ya Dar es Salaam hadi Tunduma, hatua inayokwaza biashara kati ya Tanzania na Zambia.

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamis Shaaban ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuchunguza na kuishauri serikali namna ya kuboresha matumizi ya fedha ya Zambia (kwacha) ili kupunguza ufanyaji holela wa biashara ya kubadilisha fedha hiyo katika mpaka wa Tunduma/Nakonde upande wa Tanzania na Zambia na mpaka wa Kasumulu/Songwe,