Mifuko ruksa kujenga viwanda

SERIKALI imekubali kuondoa vikwazo vinavyokwamisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza katika sekta ya viwanda.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema hayo jana mjini Dodoma wakati akifungua kikao cha Shirikisho la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini.

Waziri Mhagama amewahakikishia mameneja wa mifuko nia ya dhati ya serikali ya kuondoa vikwazo ili kusaidia mifuko hiyo kuwekeza katika sekta hiyo ili kufikia azma ya kuwa nchi ya viwanda. Mifuko itakayohusika na uwekezaji kwenye miradi mbalimbali ni pamoja na LAPF, PSPF, GEPF, NSSF, NHIF na PPF.

Katika mkutano huo wa siku moja pia ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu.

Alisema, serikali itakuwa karibu na mifuko, waratibu na Mamlaka ya Kuratibu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) katika kuchambua vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji na kuvifanyia marekebisho ili kufanikisha azma ya uwekezaji wa mifuko hiyo.

Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, uwekezaji katika viwanda utaongeza ajira kwa asilimia 40, pia utaongeza thamani katika bidhaa za viwandani, utaboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi.

Serikali inawahakikishia mifuko hiyo iliyowekeza wanakuwa na soko la uhakika na kwa kuwekeza, itaongeza wanachama na itakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, wa jamii na taifa kwa ujumla. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu aliwaeleza wajumbe wa mkutano kwamba, wizara yake ina soko la uhakika la nguo kutokana na kuwapo matumizi makubwa kwenye jeshi na kwa watu binafsi.

“Wizara imekuwa ikitumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuagiza viatu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kutumia maofisa wa jeshi wakiwamo polisi, magereza na uhamiaji, ambavyo navyo vimekuwa vikizalishwa chini ya kiwango.”

Waziri Mwigulu alisema, Idara ya Magereza imejiandaa kutengeza viatu hata kama kwa sasa inapambana na changamoto za miundombinu mibovu, uchakavu wa mashine na zinazotumika ambazo zimepitwa na wakati.

Aliongeza kwamba, Magereza wana maeneo makubwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari, hivyo Magereza wakiwezeshwa na mifuko hiyo wanaweza kuzalisha sukari kwa wingi na kusaidia kuondoa uhaba nchini.

Waziri wa Afya, Ummy alisema bajeti kwa ajili ya dawa, vifaa na vifaa tiba imeongezeka kutoka Sh bilioni 29 hadi bilioni 251, lakini fedha hizo kwa kiwango kikubwa, zimekuwa zikitumika kwa ajili ya kununulia dawa kutoka nje ya nchi.

Alisema zaidi ya asilimia 85 ya dawa, vifaa na vifaa tiba, vinaagizwa kutoka nje ya nchi kwa kutumia fedha za bajeti ambazo zinageuzwa kuwa za kigeni, hivyo kupunguza uwingi wa dawa zinazonuliwana.

Alisema soko la dawa na vifaa vya tiba nchini ni kubwa, kinachotakiwa mifuko hiyo ni kuwekeza katika kutengeneza dawa bora na zenye bei nafuu kuliko wanazoleta kutoka nje ya nchi.

Waziri Ummy aliomba mifuko mingine kuingia ubia na Mfuko wa Bima ya Afya (NIHF) kwa ajili ya kuwekeza katika kutengeneza dawa na vifaa tiba kwa sababu soko ni ndani na nje ya nchi hasa katika nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia na Malawi.