Wataka tumbaku ipewe ruzuku
- Imeandikwa tarehe 13 Juni 2012
- By Shadrack Sagati, Dodoma
- Imesomwa mara: 356
BAADHI ya wabunge wametaka Serikali ianze kutoa ruzuku ya pembejeo kwa zao la tumbaku kwa maelezo kuwa zao hilo kwa sasa linaliingizia taifa fedha nyingi za kigeni kuliko mazao mengine.
Wabunge hao Victor Mwambalaswa (CCM) na Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM) kwa nyakati tofauti walisisitiza kuwa umefika wakati sasa zao hilo lipewe ruzuku kama ambavyo Serikali inafanya kwa mazao ya chakula na pamba.
Kawawa ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Tambuku alilazimika kutoa takwimu ili kujenga hoja yake na akatoa mfano kuwa mwaka uliopita, zao hilo limeingiza kodi ya Sh bilioni 100 na kwa miaka mitatu mfululizo zao hilo limeongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni zipatazo dola za Marekani milioni 230.
Kawawa alisema kuna haja sasa Serikali kutoa ruzuku kwa wakulima wa zao hilo, ili wazalishe zaidi na wachangie katika uchumi wa taifa kwa kodi na kuingiza fedha nyingi za kigeni.
Akijibu maswali hayo ya wabunge, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alikiri kuwa tumbaku ni zao ambalo kwa sasa linaingiza fedha nyingi za kigeni hapa nchini. Lakini akasema Serikali haijaanza kutoa ruzuku kwa zao hilo kutokana na ufinyu wa bajeti.
Alisema Serikali inaendelea kuhamasisha wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika kuendelea na utaratibu wa kununulia mbolea kupitia mikopo inayopatikana kutoka benki mbalimbali.
Naibu Waziri huyo alisema utaratibu huo ni mzuri na endelevu unaomwezesha mkulima kujihakikishia matumizi ya pembejeo kwa kadri ya upanuzi wa kilimo chake na unawajengea uwezo wa kujitegemea zaidi
Akieleza ruzuku inayotolewa na Serikali, Malima alisema ruzuku inayotolewa ni ya mbegu na dawa katika zao la pamba na kupunguza bei ya pembejeo hizo. Alisema upunguzaji wa gharama za pembejeo, umesaidia wakulima kupata mbegu na kudhibiti wadudu waharibifu na kuongeza tija na uzalishaji wa pamba.
Alitoa mfano kuwa uzalishaji wa pamba umeongezeka kutoka tani 163,644 mwaka 2010/11 hadi tani 225,938 mwaka 2011/12.
Alisema changamoto za utoaji wa ruzuku kwenye zao la pamba ni pembejeo zisizokidhi viwango yaani mbegu na dawa. Alisema mkakati wa kupambana na changamoto hizo, ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa kampuni zinazouza pembejeo zisizokidhi viwango na kuwa na vikao vya mara kwa mara na kampuni za pembejeo kuhimiza kuuza pembejeo zinazokidhi viwango.


