Diageo yashinda tuzo ya utawala bora
- Imeandikwa tarehe 14 Juni 2012
- By Mwandishi Wetu
- Imesomwa mara: 330
KAMPUNI inayoongoza kwa utengenezaji wa vinywaji vyenye kilevi duniani, Diageo, imeshinda tuzo ya Utawala Bora ya Mwaka 2012 katika hafla ya utoaji tuzo za Biashara katika Afrika.
Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo kwa vyombo vya habari juzi, ilisema tukio hilo lilifanyika jijini London, Uingereza Juni 7 chini ya uratibu wa Jarida la African Business na Baraza la Biashara la Jumuiya ya Madola (CBC) na kuhudhuriwa na viongozi 300 wa Serikali, jumuiya za wafanyabiashara na wanadiplomasia.
Washindi wa tuzo hizo ni waliotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya bara la Afrika, kuwezesha kiuchumi wananchi wao na kufanya mageuzi katika taswira ya Afrika kwenye masoko ya kimataifa.
Tuzo ya Utawala Bora kwa mujibu wa taarifa hiyo, inaangalia maadili ya kibiashara, utendaji, uwazi na sera za wazi katika kupambana na rushwa.
Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Diageo Africa, Anne McCormick alisema, “jambo muhimu katika biashara ya Diageo ni dhamira yetu katika kuwa moja ya kampuni zinazoheshimika, zenye hadhi, utendaji haki na utawala bora.
Nchini Tanzania, Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) inaongoza juhudi za kujenga Mtandao Bora wa Kibiashara, ambao utasimamia maadili ya biashara na masuala ya kupambana na rushwa na maendeleo.
Kenya, Kampuni ya bia ya Afrika Mashariki (EABL) iliongoza katika kuanzisha Maadili ya Biashara nchini humo ambayo yalizinduliwa Machi.



