18Juni2013

 

Vodacom yailipa Serikali bilioni 700

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodadom Tanzania, inakadiria kuchangia Sh bilioni 130 katika malipo ya kodi kwa Serikali kwa mwaka huu wa fedha.

 

Malipo hayo yanafanya Vodacom kuwa imechangia Sh bilioni 700 tangu ilipoanza shughuli zake nchini mwaka 2001.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, malipo ya kodi kwa Serikali yamefikia zaidi ya asilimia 60 ya uwekezaji katika shughuli za Vodacom kuanzia mwaka 2001 ambayo yanafikia Sh trilioni 1.13.

Meza aliwaambia waandishi wa habari jana mjini hapa kwamba Vodacom Tanzania inayo dhamira ya kuendelea kulipa malipo hayo ya kodi kikamilifu kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari siku moja baada ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ambayo alizungumzia kwa kina jinsi Vodacom Tanzania inavyochangia ustawi wa uchumi wa Tanzania na jamii kwa ujumla.

“Hivi karibuni, tumeboresha mtandao kwa zaidi ya Sh bilioni 100 kufikia mwishoni mwa Machi mwaka huu na tunao mpango wa kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 120 ili kuendelea kuimarisha mtandao wetu,” alisema Rene.

Alisema kampuni hiyo imetoa ajira zaidi ya 450,000 ambazo zinahusisha mawakala wa M-Pesa, wauzaji wa jumla na wadogo, pamoja na waajiriwa 450.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo imetoa mchango kwa Serikali wa Sh bilioni 3.4 katika Mfuko wa Maendeleo ya Huduma za Mawasiliano Vijijini, huku pia ikijihusisha na kusaidia jamii na kuwa na mipango ya uwekezaji katika nyanja za elimu, mazingira, afya, ustawi wa jamii na wanyamapori.

“Katika miaka mitano iliyopita, kampuni imewekeza katika miradi ya huduma za jamii kupitia Vodacom Foundation, ambayo imefikia kiasi cha Sh bilioni tano,” alisema Meza na kuongeza kuwa kampuni hiyo imedhamiria kuwekeza zaidi katika miradi ya maendeleo na huduma za jamii katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema imewekeza katika masuala ya afya ya wajawazito kwa kuwekeza kiasi cha Sh bilioni 21.6 kutoka Kampuni mama ya Vodafone na Vodacom duniani.

Mbali na hayo, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Vodacom Tanzania, alisema kampuni hiyo inajivunia mafanikio makubwa katika kurahisisha huduma za kifedha kwa wananchi, kwani ndani ya mwaka mmoja kati ya 2011 na 2012, Vodacom imeshuhudia zaidi ya Sh trilioni 6.6 ya kuhamisha fedha kupitia huduma ya M-Pesa.