Wawekezaji wakwepa kodi kubanwa
- Imeandikwa tarehe 15 Juni 2012
- By Prisca Libaga, Maelezo,Arusha
- Imesomwa mara: 424
SERIKALI imeanzisha mpango wa kuwadhibiti wawekezaji na wazawa wanaokwepa kulipa kodi na kulisababishia taifa kukosa mapato ambayo yatasaidia kuboresha huduma mbalimbali za jamii na kukamilisha miradi ya maendeleo.
Hayo yameelezwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano yaliyofadhiliwa na Shirika la Mipango na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Mafunzo hayo yamekusanya wataalamu kutoka wizara mbalimbali za Tanzania bara na Zanzibar na wanajifunza mianya inayotumiwa na wawekezaji kukwepa kulipa kodi.
Masaju, amesema kutokana na kuwepo mianya hiyo mafunzo yamelenga kudhibiti miradi mikubwa ya madini ikiwemo mafuta ya petroli, na gesi ambako kunaonekana ipo mianya ya ukwepaji wa kodi.
Amesema ukwepaji mkubwa hujitokeza kwa wawekezaji katika kipindi cha mpito ambapo huwa wanabadili majina kabla ya muda wa mpito kwisha ili kukwepa kulipa kodi hivyo kuanzia sasa serikali imejizatiti kikamilifu kudhibiti ukwepaji huo.
Amesisitiza kuwa ulipaji kodi ni muhimu kwa ajili ya kuinua uchumi hivyo akawataka wawekezaji kila mmoja kuhakikisha analipa kodi ili kuwezesha taifa kusonga mbele katika kutekeleza miradi mbalimbali ambayo itasaidia kuondoa umaskini kwa wananchi.


