Wawakilishi wakatwa posho

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameridhia kukatwa posho ya siku moja ya kikao cha Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kusaidia watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Akiwasilisha hoja binafsi mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, Mohamed Said Dimwa aliwaomba wawakilishi kuchangia wananchi waliopatwa na janga hilo ambalo limesababisha vifo na mamia ya wananchi kujeruhiwa huku wengine wakipoteza makazi.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid aliwahoji wajumbe hao kufuatia hoja iliyowasilishwa na mwakilishi huyo ambapo wajumbe walikubaliana kwa kauli moja kusaidia Watanzania wenzao.

Mwakilishi wa jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said alisema janga lililowapata wananchi wa mkoa wa Kagera ni msiba mkubwa kwa wananchi wote wa Tanzania, hivyo wawakilishi wapo tayari kusaidia wananchi wenzao waliofikwa na maafa hayo.

Aidha Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele, Ali Suleiman Shihata alisema “Sisi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi posho yetu ni ndogo lakini tufanye kazi ya kuwashawishi zaidi watu wengine kuona kwamba tunapata fedha nyingi kiasi ya kufikia Sh milioni 20,” alisema.