Zuma aonya wanaoshambulia raia wa kigeni Afrika Kusini

RAIS wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amelaani kuzuka upya kwa tabia ya kuwashambulia raia wa kigeni wanaoishi nchini hapa.

Zuma amesema raia wengi wa kigeni wanaoishi Afrika Kusini, ni watu wanaoheshimu sheria na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa hilo. Amesema ni makosa kwa raia wa nchi hiyo kuwaona wageni kama ni maadui wasiofaa kushirikiana nao.

Licha ya kauli hiyo ya Zuma, waandamanaji tayari wamefunga barabara mjini Pretoria kwa kuchoma moto matairi ya magari wakijiandaa kuandamana kwa kile wanachokiita kupinga raia wa kigeni kuchukua nafasi kazi za wenyeji, hivyo kuwaongezea ugumu wa maisha.

Vuguvugu hilo la Afrika Kusini linakuja siku chache baada ya raia wa nchi jirani ya Msumbiji kufanya vurugu kubwa na kutimua raia wa kigeni nchini humo.

Miongoni mwa waathirika wakubwa wa vurugu hizo za Msumbiji ni zaidi ya raia wa Tanzania 5,200 ambao tayari wameshatimuliwa na kuripotiwa kuporwa fedha na mali zao, lakini pia Watanzania hao wakilalamikia kunyanyaswa kwa kuporwa mali, kupigwa na hata kuwapo kwa madai ya wanawake kubakwa.

Aidha, Watanzania wamelaani kwa kiasi kikubwa unyanyasaji huo, wakiwataka raia wa Msumbiji kukumbuka wema waliofanyiwa na Watanzania wakati wa harakati za ukombozi wa nchi hiyo ambayo karibu viongozi wake wote wakuu waliishi Tanzania wakati wa harakati za kupigania uhuru.