‘Dunia’ yakutana kuchangia wenye njaa milioni 5 Nigeria

WAKUU wa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa (UN) na baadhi ya nchi zenye nguvu kubwa ya kiuchumi duniani, wamekutana mjini hapa kuangalia uwezekano wa kuchangisha misaada ya mamilioni ya watu wanaokabiliwa na njaa Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Wakati wengi wa eneo hilo wamekuwa katika mateso na mahangaiko kutokana na mashambulio ya mara kwa mara ya kundi la waislamu la Boko Haram lililoweka ngome yake katika ukanda huo.

UN imelenga kukusanya kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 1.5 (sh trilioni 3) katika mwaka huu kwa ajili ya maeneo ya Ziwa Chad yanayohusisha Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, Kaskazini mwa Cameroon, Magharibi mwa Chad na Kusini Mashariki kwa Niger.

Kaskazini mwa Nigeria, moja ya maeneo yaliyokithiri kwa umasikini duniani, kwa miaka minane sasa limekuwa na machafuko kiasi cha kuathiri miundombinu ya shule, zahanati na hata sekta ya kilimo.

Aidha, raia wake wamelazimika kuyahama makazi yao kukwepa kundi katili la Boko Haram. Katika eneo hilo, karibu watu milioni 5.1 wanakabiliwa na uhaba wa chakula, huku watoto wanaokadiriwa kufikia 500,000 wakiandamwa na magonjwa ya utapiamlo.

Waziri Mambo ya Nje wa Norway, Borge Brende, akizungumza kwenye mkutano huo wa siku mbili uliofanyika juzi na jana, aliita hali ya Nigeria kuwa ni `moja ya machafuko yaliyosahaulika zaidi duniani’.

Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa UN katika ukanda huo, Toby Lanzer, naye ameelezea kusikitishwa na hali ya eneo hilo, akisema raia wake wanalazimika kupata mlo mmoja tu kwa siku, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni mchafuko yanayosababishwa na kundi la Boko Haram.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano wa Oslo ni mawaziri kutoka nchi za Ujerumani, Norway, Nigeria, Niger, Chad na Cameroon, lakini pia Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Filippo Grandi na Mkuu wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Ertharin Cousin nao wameshiriki.