Trump aahidi kuunda silaha zaidi za nyuklia

RAIS Marekani, Donald Trump amesema anataka Marekani iimarishe silaha zake za nyuklia, hiyo ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzungumzia silaha za nyuklia tangu aingie madarakani Januari 20, mwaka huu.

Amesema inaweza kuwa vyema sana iwapo hakungekuwa na taifa lolote lililo na silaha za nyuklia duniani. Lakini, amesema iwapo hilo haliwezekani, basi Marekani itahakikisha inakuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa silaha za nyuklia.

Amekaririwa akisema; “Marekani imeachwa nyuma sana katika uwezo wake wa silaha za nyuklia”. Hata hivyo, wakosoaji wanasema Marekani na Urusi tayari zina silaha za kutosha za nyuklia.

Marekani ina silaha 6,800 za nyuklia na Urusi 7,000, kwa mujibu wa chama cha udhibiti wa silaha cha Marekani.

“Mimi ndiye mtu wa kwanza ambaye angependa kuona kwamba hakuna mtu aliye na silaha za nyuklia, lakini hatutakubali kuachwa nyuma na taifa lolote lile, hata kama ni taifa rafiki, hatutaachwa nyuma katika uwezo wa nyuklia,” amekaririwa na shirika moja la habari.

Aliongeza; “Linaweza kuwa jambo zuri, ndoto nzuri endapo hakuna taifa lingekuwa na silaha za nyuklia, lakini iwapo mataifa yatakuwa na silaha za nyuklia, tutakuwa miongoni mwa wanaoongoza.”

Matamshi yake hayo yanakariri ujumbe aliouandika kwenye Twitter wiki chache zilizopita baada yake kushinda uchaguzi wa urais, ambapo aliahidi kuimarisha uwezo wa nyuklia wa Marekani.

Mkataba wa kupunguza silaha za nyuklia kati ya Marekani na Urusi, ambao unaitwa New Start (Mwanzo Mpya) unazitaka nchi hizo mbili, kufikia 5 Februari mwaka ujao, kupunguza silaha zao kwa kiasi sawa kwa miaka 10.

Chama cha udhibiti wa silaha cha Marekani, ambalo ni shirika huru lisiloegemea upande wowote, limekosoa tamko la Trump.