Bajeti PM itatoa matumaini mapya kwa Watanzania

KWA mara ya kwanza, Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano, Kassim Majaliwa amewasilisha bungeni hotuba ya bajeti kwa ofisi yake kwa mwaka ujao wa fedha huku akigusia mikakati mbalimbali iliyopangwa ili kuwaletea wananchi maendeleo kama Mwandishi Wetu OSCAR MBUZA anavyoelezea katika makala haya.

Akiwa ni msimamizi wa shughuli za serikali bungeni, hatimaye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasilisha hotuba yake ya kwanza ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha, ikiwa ni ya kwanza tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano. Pamoja na mambo mengi ya kimaendeleo, Waziri Mkuu Majaliwa amegusia mikakati ya serikali katika kuboresha utumishi wa umma, mikakati katika kupamba na rushwa na ufisadi na harakati za Taifa katika kupanua wigo wa mapato ya serikali.

Kupitia hotuba hiyo, Majaliwa pia amegusia mpango kabambe katika kushughulikia ubora wa Bandari ya Dar es Salaam, kuwasaidia wazawa katika umiliki wa biashara itokanayo na gesi asilia na pia namna inavyochukua hatua mbalimbali za kudhibiti uimara wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Akizungumzia kuhusu utumishi, Majaliwa anawataka watumishi wa umma wasio na kasoro kuendelea kuchapa kazi bila hofu, na kusisitiza kuwa itaendelea kuwashughulikia watendaji wazembe, wabadhirifu na wavivu kwa lengo la kuiwezesha nchi kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Akizungumzia Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano, Majaliwa anasema katika kutekeleza falsafa ya Hapa Kazi Tu na ili Tanzania ifikie nchi yenye uchumi wa kipato cha Kati ifikapo mwaka 2025 ni sharti kila mtu afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu wa hali ya juu.

“Ili yawepo mapinduzi ya kweli ya kuelekea kwenye uchumi wa Kati tunaodhamiria ni lazima tuimarishe uwajibikaji na maadili kwa viongozi, watendaji na kwa kila Mtanzania. Sote tumeshuhudia hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya watumishi wasio waadilifu wanaotumia fedha za umma na madaraka yao vibaya, “ anasema Majaliwa. Anaendelea kusema, “ndio maana tumeanza kwa nguvu kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha ya fedha za umma ili zielekezwe kwenye shughuli zenye manufaa kwa Watanzania walio wengi na si vinginevyo.”

Katika kusisitiza hilo, Waziri Mkuu anasema serikali itaendelea kuwawajibisha wale wote ambao hawataendana na Falsafa na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano lakini na kusisitiza kwamba serikali itachukua hatua kwa kuzingatia na kufuata Sheria, Kanuni, na Taratibu za Utumishi wa Umma.

“Niwahakikishie Watanzania kwamba hakuna mtumishi au mwananchi atakayeonewa au kunyanyaswa katika zoezi hili. Hivyo wale wote ambao wako safi waendelee kutimiza wajibu wao bila woga. Kazi zifanyike kwa weledi na kwa kasi bila urasimu,” anasema Majaliwa. Kuhusu makosa ya rushwa na ufisadi, Waziri Mkuu Majaliwa anasema wakati akihutubia Bunge Novemba 2015, Rais John Magufuli aliahidi kuwa katika mwaka 2016/2017, serikali itaanzisha Mahakama Maalumu ya Ufisadi.

“Napenda kuliarifu Bunge kwamba Serikali imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi Julai, 2016. Aidha Serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili ziweze kuharakisha utoaji wa haki,” anasema Majaliwa.

Serikali imeendelea kupambana na rushwa kwa kuchunguza tuhuma za rushwa na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya vyombo vya sheria na kwamba katika mwaka huu wa fedha, serikali imeshughulikia tuhuma 3,911 ambapo uchunguzi wa tuhuma 332 umekamilika. Kati ya tuhuma hizo, majadala 252 yaliombewa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka ambapo majalada 156 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani.

Aidha majalada 329 yaliyotokana na taarifa ya Mdhibiti na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yalichunguzwa. Majalada 19 yalikamilika na kuombewa kibali kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ambapo Majalada 12 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani. Vilevile majalada manane yaliyohusu tuhuma za rushwa kubwa yalifikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka. Kati ya hayo majalada mawili yamepata kibali na watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.

Majaliwa anaeleza kuwa miradi ya maendeleo 284 yenye thamani ya Sh bilioni 41.63 imekaguliwa katika serikali za mitaa na miradi 69 yenye thamani ya Sh bilioni 8.32 ilibainika kuwa na kasoro ambapo miradi 10 wahusika wameelekezwa kurekebisha kasoro na miradi 59 uchunguzi umeanza ili wahusika wafikishwe mahakamani. Kuhusu utekelezaji wa Sera ya Utoaji Elimu Bure kuanzia darasa la Kwanza hadi Kidato cha Nne, Waziri Mkuu Majaliwa anasema ipo changamoto ya upungufu mkubwa wa madawati baada ya kuanza kuandikisha watoto shule bila malipo.

Kutokana na hilo anawaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini waliokamata mbao kutokana na makosa mbalimbali kutozipiga mnada mbao hizo na badala yake watumie mbao hizo kutengeneza madawati pia halmashauri kutumia rasilimali zake kutengeneza madawati kwa kila shule. Waziri Mkuu anazungumzia kwa kina pia hatua zinazochukuliwa dhidi ya mapambano ya dawa za kulevya, mapambano dhidi ya Ukimwi, hifadhi ya mazingira, ustawishaji Makao Makuu Dodoma, Ushirikiano wa Kimataifa na Menejimenti ya Maafa.

Bandari, gesi, hifadhi ya jamii Kuhusu bandari anasema mkakati wa serikali ni kuhakikisha kuwa siku za uondoshaji wa mizigo bandarini unapungua hadi kufikia siku mbili au chini ya hapo ili kuongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam. Serikali imetenga aneo la ardhi la Likongo mkoani Lindi kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kuchakata gesi asilia ikiwa ni sehemu ya kutekeleza azma ya kuanza kuwaingiza wazawa katika biashara ya gesi asilia, na kueleza pia namna inavyolipa mafao ya wastaafu wakiwemo wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF.

Kuhusu Bandari, Waziri Mkuu Majaliwa anasema serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha ufanisi wa bandari zote nchini kwa kuanza na Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kuu la biashara katika Afrika Mashariki na Kati na kufuata na Bandari za Tanga na Mtwara. “Tumeanza kwa kuondoa watumishi wote wasio waaminifu ambao wanachangia kupoteza mapato ya Serikali yanayohitajika sana katika kutoa huduma muhimu kwa wananchi wetu,” anasema Majaliwa.

Vile vile Serikali imefanya kazi kubwa ya kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa kuhakikisha kwamba malipo yote yanafanyika benki na kuoanisha mifumo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania. “Niwahakikishie wananchi na wafanyabiashara kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kupunguza idadi ya siku za kutoa mizigo bandarini ili tufikie siku mbili au chini zaidi,” anasema Waziri Mkuu.

Kwa upande wa gesi asilia, anasema baada ya ugunduzi mkubwa wa gesi asilia nchini, mikakati ya serikali inayoendelea ni kubuni miradi mbalimbali hasa ile itakayoendeshwa na wafanyabiashara wazawa ili rasilimali hiyo iweze kuwanufaisha Watanzania na kuwawezesha kumiliki uchumi wa taifa lao. Serikali imetenga eneo la ardhi huko Lokongo mkoani Lindi kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kuchakata gesi asilia ikiwa ni sehemu ya kutekeleza azma ya kuwawezesha wazawa. Serikali inatarajia kuanza mradi huo katika mwaka 2016/2017.”

Kwa upande wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Majaliwa anasema serikali imeifanyia tathmini mifuko sita ya hufuma za kijamii ikiwamo GEPF, LAPF, NHIF,NSSF,PPF na PSPF kwa lengo la kupima uendelevu wake ambapo imebainika kuwa mifuko hiyo bado ni endelevu na rasilimali zake zimefikia Sh trilioni 8.8. Anasema pia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imetoa miongozo ya kupunguza gharama za uendeshaji wa mifuko hiyo itakayoanza kutumika Julai, mwaka huu.

Kuhusu Mfuko wa PSPF ambao umekuwa ukidaiwa kuwa katika hali ya wasiwasi wa uhai wake, Waziri Mkuu anasema serikali imekamilisha uhakiki wa madeni ya mfuko huo yaliyokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko huo mwaka 1999 yenye thamani ya Sh trilioni 2.9.

“Hadi sasa, Serikali imelipa sehemu ya deni la PSPF kiasi cha Sh bilioni 180 ili kuhakikisha kwamba mafao ya wastaafu wa mfuko huo yanalipwa kwa wakati. Serikali pia itaendelea kulipa deni la Sh bilioni 840.4, linalotokana na miradi ya serikali iliyogharamiwa na mifuko ya GEPF, LAPF, NHIF, NSSF na PPF,” anasema Majaliwa. Wananchi wa Maili Mbili mkoani Dodoma wametoa maoni yao kuhusiana na hotuba hiyo ya Waziri Mkuu na kusema kuwa inaleta matumaini mapya kwa Watanzania.

Hudson Mgomba anasema ni hotuba iliyoibua matumaini mapya kwa Watanzania kwa kuwa masuala ya nidhamu katika utumishi wa umma ni moja ya masuala ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele na wananchi kwa muda mrefu na kwamba suala hilo ndilo ambalo limesababisha kushamiri kwa rushwa, ufisadi na kusuasua kwa ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hata hivyo Mgomba anasema ni lazima serikali ifanye jitihada za haraka katika kuhakikisha kuwa wastaafu wa mifuko ya hifadhi ya jamii na hasa ule wa PSPF wanalipwa mafao yao haraka kutokana na wengi kuteseka kwa miaka mingi na wengine kufariki dunia bila kupata mafao yao kutokana na hali mbaya ya mfuko huo. Naye Veronica Mkuya anasema Hotuba ya Waziri Mkuu inatoa faraja kwa wananchi kwa kuwa inaeleza jinsi Serikali ya Awamu ya Tano ilivyopania kutekeleza ahadi zake kwa vitendo ili kuleta mabadiliko ya kweli.