NEC: Fanyeni kampeni kistaarabu

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wagombea na vyama vya siasa vinavyoendelea na kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani kufanya kampeni za kistaarabu zinazozingatia maadili ya uchaguzi ya mwaka 2015 na kwamba chama au mgombea atakayekiuka maadili hayo atachukuliwa hatua.

Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa NEC ,Jaji Hamid M. Hamid zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo Januari 22, mwaka huu.

Aliyasema hayo kutokana na baadhi vyama na wagombea kuanza kukiuka maadili na taratibu za kampeni kwa kutoa matamko yaliyo nje ya sera za vyama vyao.

Alisema kipengele cha maadili ya uchaguzi kinachoeleza wajibu wa vyama vya siasa na wagombea katika kuendesha shughuli za siasa wakati wa kampeni kinavitaka vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao kufanya kampeni kwa kuzingatia misingi inayolenga kutangaza sera ambazo hazijengi chuki, mfarakano na kuleta mgawanyiko katika jamii.

“Katika kampeni zinazoendelea, baadhi ya vyama vya siasa vimeanza kukiuka taratibu za kampeni na maadili na kutumia fursa ya kampeni vibaya, vinawasema viongozi wa kitaifa , kutoa matamko ambayo kihalisia siyo ya kumnadi mgombea na kufanya kampeni zisizo za kistaarabu,” alisema Jaji Hamid.

Alisema kuwa vyama au Wagombea watakaoendelea kukiuka maadili ya uchaguzi katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Tanzania pamoja na jimbo la Dimani, Zanzibar watachukuliwa hatua.

Jaji Hamid alieleza kuwa kipengele cha 5.3 cha maadili ya uchaguzi kinaeleza wazi kuwa chama au mgombea atakayekiuka maadili ya uchaguzi katika jimbo au Kata yenye uchaguzi mdogo atafikishwa katika Kamati ya Maadili ya ngazi husika na kuchukuliwa hatua stahiki.

Aidha, kipengele cha maadili ya uchaguzi yaliyokubaliwa na vyama vyote vya siasa kinafafanua kuwa kamati za maadili ya uchaguzi ngazi ya taifa, jimbo na kata katika kushughulikia malalamiko na kutoa adhabu zinaweza kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukitaka chama au mgombea kusahihisha kosa au makosa au kuomba msamaha hadharani.

Hatua nyingine ni kukisimamisha chama au mgombea kuendelea kufanya kampeni za uchaguzi, kutoza faini, kutangaza jina la chama au mgombea aliyekiuka maadili kwa kueleza kosa au makosa yake kupitia redio, televisheni, magazeti na njia nyingine za mawasiliano.