‘Hali ya upatikanaji dawa ni ya kuridhisha’

BOHARI Kuu ya Dawa (MSD) imesema hali ya upatikanaji wa dawa nchini ni ya kuridhisha.

Kwamba hadi kufikia Machi mwaka huu, upatikanaji wa dawa unategemewa kufikia asilimia 90.

Mwishoni mwa mwezi huu, dawa nyingi za aina 17 zitawasili nchini, hivyo upatikanaji wake kufikia asilimia 86 na mwezi Februari dawa nyingine za aina tatu, zitawasili na kufanya upatikanaji wqa dawa kufikia asilimia 88.

Baadaye aina nyingine mbili zitawasaili Machi na kufikia asilimia 90 ya upatikanaji wa dawa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo alisema, hali hiyo itafanya kuwepo kwa aina 100 za dawa kati ya 135 ya dawa zote muhimu.

Alisema kwa upande wa dawa za Miradi Msonge ambazo zinatibu malaria, Ukimwi, Kifua Kikuu, Ukoma, Kichaa cha Mbwa, Uzazi wa Mpango na chanjo mbalimbali zipo kwa asilimia 100 kwenye bohari za MSD huku akiwataka wateja wao kuzingatia ratiba ya uombaji ili wapatiwe kwa muda.

Aidha, katika hatua nyingine, Bwanakunu alisema, bohari hiyo imeanza utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha kuna upatikanaji endelevu wa dawa na vifaa tiba.

“Utaratibu huu unapunguza gharama za ununuzi wa dawa na vifaa tiba kutoka kwa wafanyabiashara. Hata hovyo, mpaka sasa tumeshatoa miakataba 58 ya ununuzi wa dawa muhimu mbalimbali kutoka kwa wazalishaji wa ndani na nje ya nchi,” alisema Bwanakunu.

Bwanakunu pia alisema, katika kuongeza ufanisi wake katika kupokea, kutunza na kusambaza dawa na vifaa tiba, bohari hiyo imeendelea kuboresha mfumo wa Msimbo Pau (Barcode) ambao alisema, unasaidia katika shughuli za ugavi wa dawa na vifaa tiba.

Katika hatua nyingine, Bwanakunu alisema, MSD iko katika hatua za mwisho za kumilikishwa kiwanja cha ekari 100 katika eneo la Misugusugu, Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba kupitia mpango wa ushirikishwaji wa sekta binafsi (PPP).

Alisema katika viwanda hivyo dawa na vifaa tiba mbalimbali vitazalishwa, huku akisema kuwa wanaendelea kuwakaribisha wawekezaji wanaotaka kuongeza wigo wa kuzalisha kulingana na uwezo wao wa kifedha na teknolojia.

Bohari hiyo pia ina mpango wa kufungua duka katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi mwezi huu. Bohari hiyo pia imeanzisha mpango wa huduma maalumu kwa wateja wakubwa.