Muhongo aongoza uzinduzi usanifu wa bomba la mafuta

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameongoza ujumbe wa Tanzania jijini Kampala, Uganda katika hafla ya uzinduzi wa usanifu wa awali wa bomba la kusafirishia mafuta.

Uzinduzi huo ulifanyika jijini Kampala jana, ambapo bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga, lilizinduliwa.

Mradi huo mkubwa utatekelezwa kwa ushirikiano wa serikali za Uganda na Tanzania na pia utahusisha kampuni za TOTAL, CNOOC na TULLOW.

Uzinduzi huo uliofanyika makao makuu ya Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini ya Uganda, ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri wa nchi zote mbili. Wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni makatibu wakuu wa nchi zote mbili, wakurugenzi wa mashirika ya mafuta na gesi, kampuni zilizogundua mafuta nchini Uganda za Total (Ufaransa), CNOOC (China), TULLOW (Uingereza), Kampuni ya Mafuta ya Uganda National Oil Co (UNOC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Katika uzinduzi huo, ilielezwa kuwa FEED ni moja ya hatua muhimu katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa katika viwango vinavyozingatia usalama wa kimazingira na ustawi wa jamii.

Vilevile, ilielezwa kuwa hatua hiyo itajumuisha pia upatikanaji wa njia ya gharama nafuu ya kupitisha mafuta, ambapo pia wataalamu wa taaluma mbalimbali watahusika katika kuhakikisha mradi huo unafuata viwango na ubora wa kimataifa.

Pia , imeelezwa kuwa bomba hilo, litakuwa la kwanza kwa urefu duniani kuwa bomba linalopashwa joto muda wote kutokana na asili ya mafuta yanayosafirishwa. Mradi huo wa kihistoria, una urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na unapita katika mikoa ya Kagera, Geita, Tabora, Shinyanga Dodoma na Tanga.

Mradi huo ulioridhiwa Septemba 29 mwaka jana na baraza la mawaziri, utatekelezwa nchini Tanzania mwaka huu kwa kuongeza kasi ya kukua kiuchumi. Gharama za mradi huo ni Dola za Marekani bilioni 3.5, ambapo utakapokamilika unatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 200,000 kwa siku.