TBS yaelimisha wana chuo Ardhi kuhusu viwango

SHRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu ya viwango vya ubora wa huduma na bidhaa kwa wanajamii ya Chuo cha Ardhi, Dar es Salaam, ili kupanua uelewa wao kuhusu umuhimu wa viwango hivyo, wasaidie kuisambaza kwa wananchi wengine.

Mbali na chuo cha Ardhi kilichopata elimu hiyo Januari 5 na 6, mwaka huu, shirika hilo lilikwishatoa elimu hiyo mwaka jana kwa vyuo mbalimbali nchini, kikiwemo cha Mtakatifu Augustino kilichopo Mwanza, Taasisi ya Fedha (IFM) iliyopo Mwanza, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) cha Dar es Salaam na Mwanza.

Akizungumzia elimu hiyo, Ofisa Masoko wa TBS, Debora Haule alisema huo ni mkakati endelevu wa shirika hilo la viwango nchini kuhakikisha linawatumia ipasavyo wana vyuo kueneza ujumbe muhimu wa kuthamini na kutumia viwango vya ubora kwa wazalishaji wa bidhaa na huduma, kwa sababu uwezo wa kuwafikishia ujumbe huo wanao.

Haule alisema, jambo la msingi waliloamua kuendelea kulifanya ni kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa wanavyuo, ili watumike kama mabalozi wa kushawishi wananchi wengine kununua na kutumia bidhaa zilizotengenezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, pamoja na huduma.

“Wananchi wengine wasio vyuoni tunawapa elimu pia kwa kutumia semina, redio za jamii, vipeperushi na njia nyingine mbalimbali zilizo rahisi kwao kuvielewa viwango vya ubora na umuhimu wake, lakini, tuliona ni lazima tuwe na malengo tunayoyatekeleza hatua kwa hatua kuhakikisha kila kundi linafikiwa kwa ukaribu, ndio maana tunawafuata wana vyuo vyuoni na kuwapa elimu hiyo,” alisema.

Aidha, Haule alisema kuwa shirika hilo linaendelea na mchakato wa kutafuta vibali ili kuvifikia vyuo vingi zaidi katika maeneo ya Kanda ya Kaskazini na Mashariki ya Tanzania, ambapo tayari lilikwisha tuma barua za maombi na linasubiri ruhusa ili kuanza kutoa elimu hiyo.

Katika hatua nyingine, TBS imewasisitiza wanavyuo waliopata elimu hiyo kuwaelimisha wanajamii wengine, ili wafahamu umuhimu wa kununua na kutumia bidhaa na huduma zenye viwango vya ubora, kwa sababu kufanya hivyo kutasaidia kulinda soko la ndani dhidi ya bidha zinazotoka nje ya nchi zilizo hafifu, afya za watumiaji na mazingira.