Kesi ya Dk Mvungi yaahirishwa tena

UPANDE wa Jamhuri jana umeshindwa kuwasomea maelezo ya ushahidi washtakiwa sita, wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi.

Kesi hiyo ilitajwa jana kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo hayo, lakini imeahirisha hadi Januari 23 mwaka huu itakapotajwa tena.

Kesi ilishindikana kwa kuwa upande huo wa Jamhuri, haujaondoa jina la mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Chibago Magozi (32) aliyefariki dunia akiwa gerezani.

Wakili wa Serikali, Patrick Mwita alidai hawawezi kuwasomea washtakiwa maelezo ya ushahidi, kwa kuwa hawajaondoa jina la Magozi kwenye jalada la kesi, ambalo lipo Mahakama Kuu, kwa sababu hawajapata hati ya kifo cha mshitakiwa huyo.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Thomas Simba alisema alijua watakwama kwa sababu hawajaondoa jina la Magozi kwenye kesi hiyo, halafu wakakimbilia kupeleka jalada mahakama kuu.

Wakili Mwita alidai wanaendelea kushughulikia suala hilo na tayari wameshaandika barua sehemu husika, lakini hawajapewa majibu.

Hakimu Simba alisema kesi itakapotajwa tena, upande wa Jamhuri uende na majibu ya kueleweka.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 23 mwaka huu itakapotajwa tena. Kesi hiyo ilipotajwa mara ya mwisho, Hakimu Simba aliutaka upande wa Jamhuri kuwasilisha cheti cha kifo cha mshtakiwa huyo kwa sababu jalada la kesi likipelekwa mahakama kuu, bila cheti hicho litakwama kwa kuwa hawawezi kusoma maelezo hayo hadi kwa mtu aliyekufa.

Hivi karibuni mahakama iliwaachia huru washtakiwa wanne katika kesi hiyo Masunga Makenza (40), Zacharia Msese (33), Ahmad Kitabu (30) na John Mayunga (56, kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuwa na nia ya kuendelea kuwashtaki.

Washitakiwa wanaoendelea kukabiliwa na mashtaka ya mauaji ni Longishu Losingo (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40), Juma Kangungu (29), Msungwa Matonya (30), na Masenga Mateu.