DC atoa siku 7 kwa wafanyabiashara

MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Fadhil Nkurlu ametoa siku saba kwa wafanyabiashara, kuhakikisha kuwa wanalipa asilimia 10 ya serikali inayopatikana kwenye faida zao.

Amesema wasipofanya hivyo, watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kukwepa kodi, ikiwemo biashara zao kufungwa.

Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana kuhusu ziara ya Rais John Magufuli mkoani Shinyanga.

Aliwataka wananchi wa wilaya ya Kahama, kujitokeza kwa wingi kumlaki kiongozi huyo atakapowasili.

Nkurlu alisema uchunguzi alioufanya na kamati yake ya ulinzi na usalama, umebaini kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa hawatumii mashine za kielektroniki (EFDs), hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kwa serikali kupoteza mapato yake.

Aliitaka Mamlaka ya Mapato (TRA) Wilaya ya Kahama, kupita kwa wafanyabiashara kuhakiki wafanyabiashara wanaolipa kodi ya serikali na wale wasiolipa.

“Baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa za jumla katika mji wa Kahama wengi hawatumii mashine za EFDs kutokana na uchunguzi uliofanywa na kamati yangu ya ulinzi na usalama. Hali hii inaikosesha mapato serikali. Kwa hali hiyo ninaitaka mamlaka ya mapato wilaya ya Kahama kusimamia suala hili ili kuhakikisha kuwa serikali inapata mapato yake,” alisema Nkurlu.

Alisema kuna watu wamekuwa wakiuziana majengo na viwanja na kukwepa kulipa kodi inayostahiki Wizara ya Ardhi. Wengine wamekuwa wakiuziana bila ya kufuata taratibu za kisheria kwa kuwasilisha vielelezo batili katika mamlaka husika.

Alisema katika mauziano yoyote ya vitu, lazima kuna mapato ya serikali.

Aliongeza kuna baadhi ya hoteli, ambazo zinakiuka utaratibu huo kwa kufanya biashara ya mauziano bila ya kuihusisha serikali, jambo ambalo kinyume cha Sheria.

Alisema katika mauziano ya majengo na viwanja, lazima maofisa ardhi wafanye tathmini ya asilimia 10 kwa ajili ya kuiingiza katika Serikali.

Alisema kufanya biashara bila ya kumshirikisha ofisa ardhi ni kinyume na sheria za uuzaji wa nyumba na viwanja.