Mohammed Dewji bilionea kijana zaidi Afrika

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mohammed Dewji (MO) ameng’ara na kuibuka miongoni mwa mabilionea 21 wa Afrika, huku akiwa Mtanzania pekee na kinara katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Aidha, Mo (41) ameendelea kutajwa kuwa ndiye bilionea kijana zaidi Afrika.

Katika kurudisha shukrani kwa jamii, wakiwemo Watanzania, bilionea huyo ametangaza kugawa nusu ya utajiri wake unaokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 1.4 ( Sh trilioni 3).

Juzi, jarida maarufu la uchumi duniani, Forbes lilitoa orodha ya mabilionea 21 pekee wa Afrika, tofauti na miaka mingine ambapo hutoa orodha ya matajiri 50 wa Afrika.

Kwa ujumla, mabilionea hao kutoka nchi saba za Afrika, wana utajiri wa dola za Marekani bilioni 70 ( Sh trilioni 140). Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Dewji ndiye bilionea pekee katika orodha hiyo, akishika nafasi ya 16 kati ya mabilionea hao 21.

Nafasi ya kwanza katika orodha hiyo, bado inashikiliwa na Dangote kwa mwaka wa sita sasa, akiwa na utajiri wa dola bilioni 12.1 (Sh trilioni 25.4), licha ya mwaka jana kutajwa kupata hasara ya takribani dola bilioni 5 (Sh trilioni 10.05).

Nafasi ya pili inashikwa na Nicky Oppenheimer wa Afrika Kusini mwenye utajiri wa dola bilioni 7 (Sh trilioni 14.7), akifuatiwa na Mnigeria mwingine, Mike Adenuga.

Katika orodha huyo, wamo mabilionea wawili wanawake, Folorunsho Alakija wa Nigeria mwenye utajiri wa mafuta na Isabel Dos Santos, binti wa Rais wa Angola, Eduardo dos Santos.

Isabel ndiye mwanamke tajiri zaidi Afrika, akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 3.2 (Sh trilioni 6.7).

Akizungumzia kuibuka kwake katika orodha ya mabilionea 21 Afrika, jijini Dar es Salaam jana, Dewji ambaye ni mbunge wa zamani wa Jimbo la Singida, alisema anajiona mwenye bahati. Alisisitiza ahadi yake ya kugawa nusu ya utajiri wake katika kuinufaisha jamii ya Watanzania na Afrika kwa ujumla.

Alisema utajiri alioupata, umetokana na kuungwa mkono na wanajamii wanaomzunguka, hivyo anajiona mwenye deni kila anapoona wengi wakiwa katika maisha duni.

Hii ina maana kwamba anaungana na mabilionea wengine duniani, kama Bill Gates na Warren Buffet wanaotumia sehemu ya utajiri wao kurudisha kwa jamii, wakisaidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Baada ya kushuhudia lindi la umasikini wakati nakua, nimekuwa nasononeshwa sana na hali hii, ndiyo maana ninajiona mwenye jukumu la kutaka kurudisha fadhila kwa jamii,” anaandika Dewji, mzaliwa wa Ipembe mkoani Singida katika sehemu ya barua yake ya ahadi ya kugawa nusu ya utajiri wake, iliyosainiwa Julai 15 mwaka jana.

Alisema ana lengo la kusaidia vijana na wanawake wajasiriamali wa Afrika ili nao waweze kujiimarisha kiuchumi na kusaidia wengine wasio na uwezo, kusaidia katika sekta za elimu, afya na maji ambazo kwa Afrika zinakabiliwa na changamoto nyingi.

Kwa uamuzi huo, Dewji, Rais wa mtandao wa makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Ltd (MeTL), anakuwa Mtanzania wa kwanza kuungana na kina Gattes na Buffet. Mabilionea walioamua kurudisha utajiri kwa jamii duniani sasa wamefikiria 155, wakitoka katika nchi 17.

Ameiongoza MeTL kwa miaka 17 tangu alipotoka masomoni Chuo Kikuu cha George Washington nchini Marekani mwaka 1998.

Tangu wakati huo, kampuni hiyo imekua kwa kasi, sasa ikiwa na zaidi na kampuni 31 na kuajiri zaidi ya Watanzania 28,000 nchini.

Imewekeza pia katika sekta ya viwanda katika nchi 12 Afrika. Kwa Tanzania, ndiye mwajiri wa pili baada ya Serikali.