Mwenyekiti CCM mkoa anusurika kufutwa

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Dk Jesca Msambatavangu amenusurika na uamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa huo, yaliyowafuta uanachama wanachama tisa huku wengine nane wakivuliwa uongozi.

Wanachama waliopewa adhabu hizo ni kati ya wanachama 24 wa wilaya mbalimbali za mkoa wa Iringa, waliofikishwa katika kikao hicho cha Desemba 19, mwaka jana mjini Iringa; wakituhumiwa kwa hujuma na usaliti wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Akizungumza na wanahabari jana bila kutaja majina yao, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Dodo Sambu amesema waliofutwa uanachama na kuvuliwa uongozi ni viongozi wa ngazi ya kata na wilaya.

Sambu amesema wanachama wengine wanne, mmoja kutoka Mufindi na watatu kutoka Kilolo wamepewa onyo kali, huku mwanachama mmoja kutoka Mufindi shauri lake la usaliti, likirudishwa katika kikao cha kamati siasa ya wilaya kwa uchunguzi zaidi.

“Halmashauri Kuu ya Mkoa pia ilimsamehe na kumfutia tuhuma mwanachama mmoja kutoka wilaya ya Kilolo baada ya kujiridhisha na utetezi wake,” amesema.

Amesema waliopewa adhabu hizo, bado wanayo fursa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho ya kukata rufaa kwa mamlaka ya juu ya kikao kilichowaadhibu, kama hawaridhiki na adhabu walizopewa.

Akimzungumzia Dk Msambatavangu, amesema hakufikishwa katika kikao hicho kwa sababu jina lake halikuwepo katika orodha ya watuhumiwa aliyokabidhiwa wakati akikaimishwa wadhifa huo.

“Wakati nikikabidhiwa ofisi na wakati tukifanya maandalizi ya kikao hicho, hakukuwa na jambo au taarifa yoyote niliyopewa kwa ajili ya kufikishwa katika kikao hicho ikumhusu mwenyekiti wa mkoa,” amesema Sambu, anayekaimu wadhifa huo uliokuwa ukishikiliwa na Hassan Mtenga, ambaye hivi karibuni alihamishiwa mkoa wa Pwani.

Sambu amesema hata kama taarifa za kiongozi huyo wa mkoa, zingefikishwa katika kikao hicho, wasingeweza kutoa adhabu yoyote kwake, kwakuwa mamlaka hiyo kikatiba ni ya vikao vya Taifa.

Desemba 24, 2015 Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa wa Iringa ilitangaza mbele ya wanahabari majina ya makada wake 102 akiwemo mwenyekiti huyo, ikiwatuhumu kukisaliti na kukihujumu chama wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Majina hayo yalitangazwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Dk Yahaya Msigwa, ikiwa ni wiki moja tu baada ya vijana wa chama hicho waifungie ofisini kwa zaidi ya saa mbili kamati hiyo, iliyohudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika ofisi za mkoa za chama hicho, mjini Iringa.

Machi 24, 2016 Msambatavangu alizungumza na wanahabari na kufichua mpango aliouita haramu wa kumng’oa madarakani, akisema unaratibiwa na wajumbe wawili wa kamati ya siasa ya mkoa huo pamoja na aliyewahi kuwa waziri katika awamu moja ya serikali zilizopita, kwa kutumia tuhuma za uongo za kukisaliti chama.

Akiapa kupigania haki yake ndani ya chama hicho, alisema uongo na uzushi huo, ulikuwa unatungwa dhidi yake kwa lengo la kuwalinda viongozi mbalimbali (hakuwataja) wanaodaiwa kuutumia uchaguzi huo kujipatia maslai binafsi.

“Lakini pia wajumbe hao wanataka madaraka ndani ya chama kwa kutumia mbinu hizo chafu,” alisema huku akiahidi kuwashitaki katika ngazi ya Taifa viongozi hao.