Kuku wapunguza umasikini Chamwino

MRADI wa uendelezaji na uboreshaji wa kuku wastahimilivu katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara umeendelea kutekelezwa katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Kuku kutoka Ethiopia na Malawi wamegawiwa kwa wakulima ili kuangalia uzalishaji na aina ya kuku inayokubalika kwa wafugaji.

Kuku hao ni aina ya sasso na kroiler wenye uwezo wa kutaga mayai 200 hadi 280 kwa mwaka.

Ofisa Ugani wa Kata ya Buigiri wilaya ya Chamwino, Miriam Zablon amesema leo kuwa, utekelezaji wa mradi huo ulioanza Julai mwaka jana unaendelea vizuri ambapo umesaidia kupunguza umasikini kwenye kaya.

Amesema wakulima wanaonufaika na mradi huo ni wale wa maeneo ya Chamwino, Ikulu, Chalinze, Makanwa na Buigiri.

Miriam amesema, mradi huo uko kwenye utafiti na kwamba, wakulima 40 kila kijiji walipewa kuku 25 wa wiki sita ambao wamepata chanjo zote muhimu kama mdondo, gomboro, ndui na typhoid.

“Kwenye mradi huu tunategemea kwamba wiki ya 20 jogoo anakuwa na kilo mbili hadi sita huku majike yakitakiwa kuwa na kilo mbili hadi kilo tatu na nusu,” alisema.

Amesema asilimia 75 ya wanufaika wa mradi huo ni kinamama.

“Kabla ya mradi kuanza tuliwaelimisha wakulima kuwa kama watakuwa wafugaji watakaohusika kwenye utafiti watapewa kuku wasiopungua 25 wenye umri wa wiki sita na kufanya kazi kwa kushirikiana na mtaalamu atakayekuwa akichukua takwimu kijijini,” amesema.

Alisema takwimu hizo ni pamoja na uzito wa kuku, uzalishaji wa mayai,gharama zinazotumika kuwatunza na mapato yanayopatikana kwa kuuza mayai.

Aidha amesema kuku wa hapa nchini wana uwezo wa kutaga mayai 60 hadi 80 kwa mwaka na ujio wa aina ya kuku wenye kutaga mayai mengi utaimarisha uchumi kwenye kaya kwani mkulima anaruhusiwa kuuza majogoo na mayai.

Mkazi wa Buigiri Aksa Kamanjezi amesema mradi huo umekuwa na manufaa kwake kwani licha ya kupata lishe bora amekuwa akiuza mayai na majogoo ambapo jogoo mmoja amekuwa akiuza kwa Sh. 25,000.