RC azuia wanafunzi kurudishwa nyumbani

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameagiza walimu kutowarejesha wanafunzi nyumbani kwa kukosa sare.

Amewataka walimu hao kuhakikisha kwamba wanafunzi hao wanasoma kufikia malengo ya taifa la kuwa na wataalamu wake.

Pia amewataka watumishi wa Afya kuacha kutoa lugha chafu kwa wazee na wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu hospitalini.

Gambo ametoa maagizo hayo nyakati tofauti katika ziara wilayani Karatu.

Akihutubia wananchi kijiji cha Oldean amesema shule zimeshafunguliwa na asingependa kuona mwalimu yoyote anawarudisha wanafunzi majumbani kwa kukosa sare za shule au kutokamilisha baadhi ya vitu muhimu kwa ajili ya masomo yao.

Amesema, pamoja na serikali kuondoa michango isiyo ya lazima kwa wazazi au walezi iwapo kunaonekana ulazima ni vyema kupitisha hoja katika vikao husika ili kuleta maendeleo shuleni pamoja na wanafunzi.

Pia ametoa rai kwa wazazi na walezi kufuatilia kwa makini mienendo ya watoto wao mashuleni ikiwemo kuhakikisha wanawanunulia sare za shule ili waweze kupata elimu sambamba na kuwanunulia mahitaji yao muhimu.

Wakati huo huo, Gambo amewasihi watoa huduma za afya kuacha tabia ya kuwatukana wazee hospitalini au kwenye zahanati wanapokwenda kupata matibabu na kusisitiza madirisha ya wazee ni lazima yaheshimiwe.

Mmoja kati ya wananchi hao, Salome Shauri anayeishi Kitongoji cha Darajani alimuomba Mkuu wa Mkoa kufika kijiji kwao kwa ajili ya kupata msaada wa kupimiwa ardhi yake iliyomegwa na jirani yake kwa ajili ya kupitisha njia ya mifugo.

Pia walihoji ni kwa nini hawajasomewa mapato na matumizi ya kijiji hicho tangu mwaka 2012 hadi mwaka huu huku fedha za wananchi na za wawekezaji zikiwa zinakusanywa.

Gambo amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Waziri Morice kutuma wataalamu wake siku ya Jumatatu ijayo kwa ajili ya wananchi hao kupewa taarifa za ukaguzi wa mapato na matumizi ya kijiji hicho sanjari na kupewa elimu ya mikopo kwa kinamama na vijana ili waweze kuendesha biashara zao.