Mke mdogo ajinyonga mume akiwa kwa mkubwa

MKAZI wa kijiji cha Miyogoni, kata ya Mbugani, manispaa ya Tabora, Mwajuma Hamad, amejinyonga usiku wa kuamkia jana huku sababu za kujinyonga kwake zikiwa hazijulikani.

Mtoto wa mwanamke huyo, Tatu Juma, alieleza kuwa walienda kulala na mama yao na wakati wa usiku, mdogo wake alitaka ampeleke kujisaidia na ndipo alipoanza kumuita mama yake pasipo kuitikiwa.

Mume wa marehemu, Juma Kiligito, alieleza kuwa akiwa amelala na mke mkubwa ndipo majira ya asubuhi, alipoamshwa na mtoto wake aliyemweleza kuwa mama yake amejinyonga.

Kiligito alisema hapakuwa na ugomvi wowote kati yake na mkewe huyo na alisema usiku walikuwa wote wakizungumza hadi saa tano wakiwa wanaangalia runinga.

Mke mkubwa wa Kiligito, Asha naye alisema hawakuwa na tatizo na marehemu na kwamba walikuwa wakiangalia runinga wote usiku na baadae kila mmoja kwenda kulala yeye akiwa na mumewe.

Hata hivyo mama mzazi wa marehemu, Sada Said, alieleza kuwa siku moja kabla ya kifo chake, mtoto wake (marehemu) alienda kumlalamikia mumewe kuwa hataki ajishughulishe ili kupata kipato.

Alisema mwanawe alimfuata majira ya saa 10 jioni akimweleza kuwa mumewe hataki ashone wakati hali ya maisha ni ngumu kwa vile alikuwa na watoto na wana mahitaji mengi ya kifamilia yanayohitaji fedha.

Alieleza kuwa walimsihi arudi nyumbani kwake na yeye (mama) na kaka wa marehemu, wangeenda kuwakutanisha na mumewe na kufahamu kwa nini alikuwa hataki ashone ili kuingiza kipato cha familia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa, alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa Polisi inalichunguza.

Issa alisema Polisi inafanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mwanamke huyo kujinyonga na aliwataka wananchi wa eneo husika lilipotokea kifo hicho, wawe watulivu wakati uchunguzi ukiendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, amewataka wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia Polisi katika uchunguzi wao wajitokeze kusaidia.

Mwanri amesema ikiwa taarifa zaidi na sahihi zitatolewa mapema kwa vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Polisi, itasaidia uchunguzi kukamilika kwa muda mfupi.