CCM yazoa vijiji 10 kati ya 11 Chamwino

UCHAGUZI wa wenyeviti wa serikali za vijiji vipya katika wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma umemalizika huku Chama Cha Mapinduzi(CCM) ikishinda katika vijiji 10 kati ya 11.

Katika uchaguzi huo uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita, vijiji vilivyofanya uchaguzi kwa mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa serikali ya kijiji na wajumbe wa viti maalumu.

Vijiji vilivyofanya uchaguzi huo ni Chamhumba, Mwendomela, Kazaroho, Mguba, Bwawani, Umoja, Mbelezungu, Chitabuli, Malecela, Mlazo na Muheme.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chamwino, Charles Ulanga, katika matokeo ya jumla CCM ilishinda nafasi ya uenyekiti katika vijiji 10 kati ya 11.

Alisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ilishinda kijiji kimoja cha Champumba. Ulanga alisema uchaguzi huo ulichagua wenyeviti wa serikali ya vijiji, wajumbe wanane wa serikali ya kijiji, wenyeviti wa vitongoji na wajumbe wa viti maalum ambapo jumla yao wanatakiwa kuwa 25.

Uchaguzi huo ambao matokeo yake yalitangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Athumani Masasi, ulihusisha vijiji vipya vya wilaya hiyo vilivyoanzishwa mwaka 2015.