Majaji, Mahakimu wafagilia sheria ya uhujumu

CHAMA cha Majaji na Mahakimu Mkoa wa Manyara (JMAT) kimeunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na ujangili katika hifadhi mbalimbali za Taifa kwa kufanya mabadiliko ya sheria za wanyamapori na uhujumu uchumi.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Salma Maghimbi, alisema kuwa mabadiliko katika sheria za uhujumu uchumi na sheria mbalimbali yaliofanyika mwaka 2016 yaliwezesha kuanzishwa kwa divisheni maalum ya mahakama kuu kwa ajili ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi ambayo ni mahakama ya mafisadi.

Alisema mabadiliko pia katika sheria za wanyamapori kuwa makosa ya uhujumu uchumi ni hatua ambayo ilionesha jinsi masuala hayo yana madhara kwenye uchumi.

Aliyasema hayo katika ufunguzi wa Mkutano mkuu wa kwanza wa JMAT uliowakutanisha mahakimu wa ngazi zote wa mkoa na wadau wa mahakama mkoa wa Manyara ili kuzungumza nao juu ya utendaji kazi wa mahakama.

Mwenyekiti wa JMAT Tawi la Manyara, Elimo Massawe alisema kuwa mkutano huo ulijikita katika kujadili sheria za wanyamapori, ukamataji, upelelezi, uhifadhi na utoaji vielelezo mahakamani pamoja na maadili kwa maofisa wa mahakama.

Alisema mkutano huo utabadilisha utendaji kazi wa wanachama wa JMAT kitaaluma na kimaadili na kuifanya kanda ya Arusha kuendelea kuwa kanda bora kiutendaji kwa kuwa wataweza kubadilishana ujuzi na utendaji na wadau wengine wanaoshirikiana nao, wakiwemo waendesha mashtaka, jeshi la Polisi na wataalamu wa masuala ya wanyamapori.

Akifunga semina hiyo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera, alifafanua kuwa mahakimu na majaji ni wasimamizi wakubwa wa sheria za nchi na kwamba ana imani kuwa watasaidia kusimamia upatikanaji wa ufumbuzi wa changamoto za hifadhi ya misitu na wanyamapori ambao mkoa huo umekuwa ukiongoza kwa changamoto hizo.

Alizitaja changamoto katika hifadhi ya misitu na wanyamapori ni pamoja na kasi kubwa ya ukataji miti katika misitu ya hifadhi, uchomaji holela wa misitu, mauaji ya wanyama na uvamizi wa maeneo katika hifadhi. Alisema mahakama inayo nafasi ya pekee katika mfumo wa kutoa haki nchini na kwamba watu wanapokwenda mahakamani wanategemea kutendewa haki.

“Matarajio ya wananchi ni kuwa kesi zisicheleweshwe kusikilizwa na kuamuliwa pale ambapo upelelezi umekamilika na mashataka yametayarishwa vizuri kuahirishwa kusikilizwa kwa kesi huzaa manung’uniko,” alisema Dk Bendera.

Dk Bendera aliwakumbusha mahakimu na majaji kuwa mahakama ni kilele cha mfumo wa utoaji haki nchini lakini mahakama haipelelezi, haifikishi wahalifu mahakamani na haiendeshi mashtaka hivyo wapelelezi, waendesha mashtaka na wanaotetea wasipofanya kazi yao ipasavyo haki itacheleweshwa.

“Mipango yenu ilenge katia kutatua changamoto hizo na si kuongeza migogoro ili kuhakikisha changamoto hizo zinaisha kila mtendaji awajibike kwa kiwango cha juu katika nafasi yake kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Bendera.

Alisema hatua hiyo ina maana kuwa polisi wahakikishe wahalifu wanakamatwa, upelelezi unafanyika kwa makini na kesi zao zinapelekwa mahakamani na kuwataka waendesha mashtaka nao wahakikishe mashauri wanayoyawasilisha mahakamani yameandaliwa vizuri ili yachukue muda mfupi kusikilizwa na kuamuliwa.