RC aagiza walimu warudishiwe fedha

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo kuhakikisha fedha za walimu wa shule za sekondari na msingi zilizokatwa na halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya vitambulisho vya kazi, zinarudishwa.

Gambo ametoa agizo hilo leo wilayani Karatu wakati alipokuwa akizungumza na walimu hao kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Karatu (Karatu Boys) kujua matatizo wanayokutana nayo na jinsi ya kuyatatua, ikiwemo madeni ya likizo na upandaji wa madaraja.

Amehoji ni kwa nini walimu wakatwe Sh 6,000 kwa ajili ya kutengenezewa vitambulisho vya kazi wakati ni haki yao kama watumishi na waajiriwa wa halmashauri hiyo kupata vitambulisho vya kazi bure.

Amemwagiza Mahongo kuhakikisha anafuatilia na kuchukulia hatua watumishi wa halmashauri hiyo waliowakata walimu hao wa msingi na sekondari kiasi hicho cha fedha, na kuwachukulia hatua.

"Eti vitambulisho vyenu mmetozwa hela kwa sababu gani wakati ni bure, sasa nasema aliyehusika na kuwatoza Sh 6,000 kwa ajili ya vitambulisho vyenu vya kazi atachukuliwa hatua … hii siikubali," amesema Gambo.

  Amewaondoa hofu walimu hao kuwa serikali ya mkoa wa Arusha itahakikisha kuwa madeni yote wanayodai yatashughulikiwa ili waweze kufundisha vyema wanafunzi.

Awali, walimu hao baadhi walisema wengine wanatembea umbali mrefu kwa ajili ya kutoa elimu huku wanafunzi nao kwenye baadhi ya shule wakishindwa kuhudhuria masomo yao kwa wakati sababu njiani wanakutana na wanyamapori.

Pia mwalimu Joakim Petro akisema awali alisimamishwa kazi kwa mizengwe na baadaye kurudishwa kazini na kuamriwa kupewa Sh milioni 3. 5 kama madai ya usumbufu na mishahara yake lakini tangu mwaka juzi hajapewa fedha zake.

Pia fedha za walimu za Saccos zaidi ya Sh milioni 11.3 ambazo ni makato yao hawazioni na hata wakitaka kuzikopa wanaelezwa hazimo sasa zimekwenda wapi.

Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mahongo alisema anafuatilia suala hilo ili kujua ni mtumishi gani wa halmashauri alichukua fedha hizo kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Waziri Morice ili kuchukua hatua kali za kinidhamu.