CCM- Kumchagua mgombea upinzani hasara

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewaomba wananchi wa kata ya Matevesi, wilayani Arumeru kumchagua mgombea udiwani kupitia chama hicho ili aweze kuwatatulia kero za zahanati, maji na barabara kwa kuwa atakuwa na mawasiliano ya karibu na serikali iliyoko madarakani.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Juma Idd alipozungumza katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata hiyo.

Alisema kuwa ni hasara kumchagua mgombea wa chama kingine kisicho na serikali.

Amesema mpaka sasa serikali iliyoundwa ni ya CCM kwa hiyo kila jambo linalofanya liko katika Ilani ya chama hicho ambapo itakuwa vigumu kwa diwani wa upinzani kuisimamia kwa kuwa hata kitabu cha Ilani kina rangi ya kijani na ataona aibu kuitekeleza.

Amesema kutokana na sabahu hizo ipo kila haja ya kumchagua mgombea wa CCM kwa ajili ya manufaa yao na kuachana na ushabiki usio na msingi wowote kwakua hakuna atakayepata hasara kwa kuuchagua upinzani na kukosa maendeleo isipokuwa wao wenyewe wakazi wa kata hiyo.

Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Arusha, Michael Lekule Laizer amesema wananchi hao hawapaswi kubabaika katika uchaguzi huo mdogo bali kumrejesha madarakani diwani Sovoyo ambaye tayari alishaanza majukumu yake na Ilani anayo tayari.

Alisema ipo sababu ya kuunganisha nguvu kwa diwani huyo kati yake na mkuu wa wilaya hiyo katika kutatua kero zinazowakabili wananchi wake.

Laizer aliongeza kwa sasa viongozi wawakilishi wa wananchi wana kazi ngumu ya kuonana na wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, mawaziri na hata waziri mkuu na rais katika kuwasilisha matatizo ya wananchi wao, hali ambayo hapendi iwakute wakazi wa Matevesi kwa kumchagua diwani wa upinzani.

Akizungumza katika mkutano huo mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa na mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo, Alexandar Mnyeti kuzungumza na mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha kuanza kazi mara moja ya ukarabati wa barabara.

Alitoa agizo hilo kama mkuu wa mkoa baada ya kupita na kuona mkutano huo na ambapo alipenda kusikiliza kero za wananchi ambao walilalamikia mambo hayo na yeye alipaswa kutolea majibu kero hizo kwakua zipo mashine za halmashauri za ukarabati huo wa barabara.

Aidha aliwaambia wakazi wa kata hiyo kuwa watahakikisha wizi wa kura wa aina yoyote hautokei, ikiwemo kuwadhibiti wale wote walioandaliwa kuja kupiga kura ilihali si wakazi wa kata hiyo, lakini pia kuwadhibiti wale wote waliojipanga kufanya vurugu siku ya uchaguzi.