Mmiliki gesti anyweshwa, aibiwa

POLISI mkoani Rukwa inawasaka wageni waliofikia katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Mbilinyi Guest House iliyopo katika manispaa ya Sumbawanga kwa tuhuma za kumwibia mmiliki wa nyumba hiyo vitu na fedha taslimu, vyote vikiwa na thamani ya Sh 914,000 baada ya kumnywesha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , George Kyando amesema wizi huo ni wa Januari 9, mwaka huu saa mbili usiku katika nyumba hiyo ya kulala wageni ya Mbilinyi.

Amemtaja mmiliki wa nyumba hiyo ambaye pia ni mkazi wa eneo la Majengo, manispaa ya Sumbawanga kuwa ni Tumain Mbilinyi (32) ambaye aliibiwa TV mbili za nchi 24 za thamani ya Sh 600,000 na fedha taslimu Sh 314,000 na watu ambao walikuwa ni wapangaji katika nyumba hiyo.

“Uchunguzi wa awali wa kipolisi umebaini kuwa watu hao waliokuwa wamepanga vyumba katika nyumba hiyo ya kulala wageni waliwapatia vimiminika vinavyosadikiwa kuchanganywa na dawa za kulevya mhudumu wa nyumba hiyo, mlinzi na mhudumu wa kike wa baa ya Uyole," amesema Kamanda.

Kamanda alisema mhudumu huyo wa baa ya Uyole ndiye aliyeenda na watuhumiwa hao katika nyumba hiyo ambapo waliwanywesha hadi kulewa na kutumia mwanya huo kuiba vitu hivyo vya thamani ya Sh 914,000.

Kyando aliwataka wahudumu na walinzi wote wa mahoteli, baa na nyumba za kulala wageni kuwa makini na kuacha tabia ya kupokea vyakula, vinywaji au kitu chochote wawapo kazini hasa kwa watu wasiowafahamu.

Alisema watuhumiwa hawajakamatwa na jitihada za kuwasaka zinaendelea ili wakikamatwa sheria ichukuwe mkondo wake.