DC aingilia kati sakata la wafugaji na Maliasili

MKUU wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Peres Magiri ameingilia kati sakata la mgogoro wa wafugaji na maofisa maliasili wilayani humo baada ya wafugaji 4 kukamatwa na kuswekwa ndani.

Mmoja kati ya wafugaji hao alipigwa risasi na kuvunjwa miguu yake kwa madai ya kuingia katika eneo la hifadhi.

Sakata hilo ambalo limeibua hasira miongoni mwa wafugaji limemfanya mkuu huyo wa wilaya kukutana na wafugaji wote wa vijiji vilivyoko katika kata ya Ngoywa na Ipole wilayani humo na kusikiliza malalamiko yao huku akiahidi kuchangia gharama za matibabu kwa mfugaji aliyepigwa risasi.

Awali alikutana na viongozi wa chama cha wafugaji wilayani humo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kanda ya Magharibi, Kusundwa Wamalwa ambao walieleza kusikitishwa kwao na vitendo vya kamatakamata, udhalilishwaji, vipigo na uonevu wanavyofanyiwa na askari wa maliasili.

Peres Magiri aliwaambia wafugaji hao kuwa serikali haina dhamira ya kumnyanyasa mwananchi wake na hata inapotokea kuna tatizo eneo fulani kiongozi anapaswa kukutana na wahusika na kusikiliza malalamiko yao na kuyafanyia kazi.

Alisema ili kubaini ukweli wa malalamiko yao, ikiwemo vipigo, kukamatwa wafugaji na mifugo ndani au nje ya eneo la hifadhi, DC ameunda kamati itakayochunguza ukweli ili kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua.

Aidha aliwataka kufuata taratibu punde mifugo yao inapokamatwa na sio kutozwa mamilioni ya faini na askari hao pasipo kufuata mwongozo au utaratibu unaokubalika wa ulipaji faini.

Alitaja viwango vya faini vinavyopaswa kutozwa kwa mifugo inayokamatwa, kuwa kila kundi la ng’ombe 2-10 faini ni Sh laki 2 na fidia milioni 1 (jumla mil 1.2), kundi la ng’ombe 11-50 faini ni Sh laki 5 na fidia 2.5 (jumla Sh mil 3) na ng’ombe 51-100 faini ni laki 7 na fidia Sh milioni 3.5 (jumla Sh mil 4.2) na sio vinginevyo.

Aliongeza kuwa ng’ombe kuanzia 100 na kuendelea faini yake inakuwa milioni 1 na fidia milioni 5 jumla Sh mil.6, aidha alisema ofisa wanyamapori yeyote atakayebainika kutoza faini na fidia zaidi ya kiwango kilichowekwa sheria itachukua mkondo wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Simon Ngatunga alisema wafugaji ni wadau muhimu sana kwa maendeleo ya halmashauri yake, kwani wamekuwa wakichangia fedha nyingi kwa shughuli za maendeleo ya wilaya hiyo.

Alimwagiza Mtendaji wa Kata na Wenyeviti wa serikali za vijiji kukaa meza moja na wafugaji hao na kusikiliza kero zao na kama kuna tatizo kubwa walilete ofisini kwake haraka ili lishughulikiwe kuliko kusubiri hadi mtu apigwe risasi au akamatwe.