RC Gambo aomba msaada TASAF

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameagiza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) Mkoa wa Arusha kusaidia ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu kupunguza msongamano kwa wanafunzi pamoja na kuongeza idadi ya walimu maeneo ya pembezoni.

Gambo alitoa rai hiyo jana kijiji cha Lositete wakati akiweka jiwe la msingi la nyumba ya walimu ya familia mbili iliyofadhiliwa na Tasaf kwa gharama ya Sh, 98,145,800.

Alisema maeneo hayo ya pembezoni yanahitaji maendeleo mbalimbali ikiwemo kuibuliwa kwa miradi ya Tasaf itakayosaidia kaya maskini kujikwamua kiuchumi kwa sekta ya afya, kubuni miradi mbalimbali pamoja na miradi mingine ili kunusuru kaya masikini.

Alisema Tasaf Mkoa wa Arusha inajitahidi kuhakikisha inahudumia kaya maskini kwa kusaidia wananchi wanaoishi kwenye mazingira magumu kujikwamua kiuchumi kwa kubuni miradi mbalimbali iyakayowasaidia kujikwamua kuuchumi.

Alisema nyumba hiyo ya walimu itasaidia kuwezesha walimu kutoa elimu bora kwa wanafunzi ikiwemo kutatua changamoto ya utoro shuleni.

"Nawaomba Tasaf muangalie maeneo haya ya pembezoni kwani yanahitaji maendeleo mbalimbali, ikiwemo elimu hapa Tasaf ni bora kuongeza idadi ya madarasa na nyie wananchi mbuni miradi ya kujikwamua kuuchumi na kuondokana na umaskini."

Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) Mkoa wa Arusha, Mathias Seif ametoa rai kwa wananchi wa wilaya hiyo na vijiji vyake kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo ili kujikwamua kiuchumi na Tasaf inatoa fedha au miradi kwa kaya maskini, ikiwemo maeneo ya pembezoni.