Makamba awapongeza watendaji kulinda mazingira

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano (Muungano na Mazingira), January Makamba amewapongeza watendaji wa Wizara ya Kilimo na Maliasili ya Zanzibar kwa juhudi wanazozichukuwa katika kulinda mazingira ya misitu na vyanzo vya maji visichafuliwe na binadamu.

Makamba alisema hayo wakati akifungua kituo cha Hifadhi ya Maumbile cha Msitu wa Masingini ambacho kitakuwa kikitumika kwa ajili ya kulinda hifadhi ya mazingira na watalii.

Alisema kazi ya kulinda mazingira na uhifadhi wa msitu pamoja na vyanzo vya maji ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 ikiwa na lengo la kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo vinafaidika na rasilimali hizo muhimu.

Alisema kwa mfano uhifadhi wa msitu kwa sasa ni moja ya vyanzo vizuri vya kuingiza mapato ambapo katika baadhi ya nchi zinatumia rasilimali hiyo katika kukuza sekta ya utalii kama kivutio kwa wageni.

"Miongoni mwa utalii ambao umepata umaarufu mkubwa duniani ni wa uhifadhi wa msitu kwa ajili ya kupata hewa safi," alisema Makamba.

Alisifu juhudi za ubunifu wa hali ya juu uliofanywa na wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ambayo sasa imebadilisha kabisa sura ya eneo la msitu wa Jozani na kuufanya kuwa kivutio kikubwa cha utalii.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Ali Juma Ali aliwataka wananchi waliozungukwa na msitu wa hifadhi ya Jozani kuwa walinzi wazuri na kuepuka uharibifu ikiwemo ukataji wa miti.

Alisema kituo hicho kipo katika maandalizi ya kuweza kuwatambua na kuwasajili wanavijiji wote wanaoishi na kuzungukwa na msitu huo wa ajili ya kunufaika mapato yanazalishwa hapo ikiwemo malipo ya watalii.

"Tunataka kuwashirikisha kikamilifu wanavijiji wanaoishi na kuzungukwa na msitu huu kuona kwamba ni wao na upo kwa ajili ya kuimarisha mapato yao," alisema.

Alisema utaratibu kama huo upo kwa pande wa msitu wa Jozani Unguja ambapo katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya Sh milioni 60 zimekusanywa na kugaiwa kwa wanavijiji wanaozungukwa na msitu huo ikiwa ni sehemu ya pato lao.

Eneo la msitu wa hifadhi ya Masingini wenye ukubwa wa hekta 566 umezungukwa na shehia 10 zenye wakazi laki tatu ambao kwa njia moja walikuwa wakitumia msitu huo kwa shughuli mbali mbali za kijamii.