Bilal ashauri kuachwa kwa mila potofu

MAKAMU wa Rais mstaafu wa Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilali amewataka wazazi wa kijiji cha Mgonjoni mkoa wa Kaskazini B Unguja kuacha mila potofu na kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule kupata elimu ya msingi ambayo kwa sasa ni ya lazima.

Dk Bilali alisema hayo wakati akifungua majengo ya shule ya msingi ya Mgonjoni ambayo kukamilika kwake sasa kutawawezesha watoto kupata elimu kwa kupunguza umbali wa kutembea.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo yalipelekea kuwepo kwa Mapinduzi ya mwaka 1964 ni wananchi wa wazalendo kukosa moja ya haki na fursa ya elimu wa maendeleo ya taifa. Alifahamisha kwamba elimu ilikuwa ikitolewa kwa misingi ya makundi ya matabaka ya watu wa aina fulani tu huku wazalendo wakiishia katika elimu ya msingi tu.

"Hizo ndiyo sababu zilizosababisha viongozi wetu waasisi kufanya Mapinduzi ya Januari 1964. Tulikoseshwa elimu ambayo ilikuwa haki yetu," alisema Dk Bilali.

Alisema ni aibu katika karne hii ya sayansi na teknolojia wakati Zanzibar inaadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Januari 1964 kuwepo wazazi ambao hawapo tayari wapeleka shule watoto wao.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alisema wamejipanga kuhakikisha kwamba wanapokea watoto wote waliofikisha umri wa kuanza shule ya maandalizi Unguja na Pemba.

Alifahamisha kwamba sera ya wizara hiyo kwa sasa ni kuhakikisha elimu ya maandalizi inakuwa ya lazima ili kuwaweka vizuri wanafunzi kuingia katika elimu ya msingi wakiwa tayari katika mazingira mazuri.

"Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inasisitiza kwamba elimu ya maandalizi ni ya lazima kwa hivyo wazazi wanapaswa kupeleka watoto wao shule na hakuna vikwazo dhidi yao," alisema.

Mapema Dk Bilali alizindua vitabu vitakavyotumika kwa ajili ya masomo ya Kiingereza kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tano. Riziki alisema katika mikakati ya kuimarisha elimu ya mwaka 2017-2020 suala la upatikanaji wa vitabu vya kusomea kwa wanafunzi limepewa kipaumbele cha kwanza. "Tumeweka malengo kuhakikisha kwamba kila mwanafunzi anakuwa na kitabu chake mwenyewe ili uweza kusoma vizuri," alisema.