Ewura, mamlaka bora mashariki na kusini mwa bara la Afrika

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangazwa kuwa mamlaka bora ya udhibiti wa huduma za maji na usafi wa mazingira katika nchi za mashariki na kusini mwa Afrika kwa kuzingatia mipango ya utawala bora katika udhibiti.

“Ewura imekuwa na mipango thabiti katika kutimiza majukumu yake mbalimbali ya udhibiti kwa kuzingatia utawala bora hivyo inafaa kuwa kiongozi barani,” inasema ripoti ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini (Esawas).

Matokeo hayo ya ripoti yaliwasilishwa Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika kwa muda wa siku tatu wa Esawas inayojumuishwa na wanachama saba ambao ni mamlaka za udhibiti wa huduma za maji na usafi wa mazingira kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Msumbiji, Zambia, Lesotho, Burundi na Tanzania.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ewura imekuwa mdhibiti bora kwa kutimiza wajibu wake wa kiudhibi kwa kuzingatia utawala bora, hii inatokana na sheria kuweka wazi kanuni, wajibu na majukumu ya Ewura katika kuhakikisha inaimaraisha misingi ya kudumu na kiini cha mfumo mzima wa udhibiti.

Pamoja na hayo, Ewura ni Mamlaka ya Udhibiti inayosimamia mamlaka nyingi za huduma za maji kwa kusimamia jumla ya mamlaka 130, ikiwa ni idadi ya juu kabisa ikifuatiwa na Kenya 103, Zambia (18), Msumbiji (15) na Rwanda, Burundi na Lesotho ina moja kwa kila mmoja.

Pamoja na mambo mengine, ripoti inasisitiza kuwa sheria inapaswa kumuwezesha mdhibiti kutekeleza maamuzi yake kuweka mamlaka ya kukokotoa bei, kufuatilia mwenendo wa sekta zinazodhibiti na kuweka kanuni na sera katika sekta hizo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ESAWAS sheria inapaswa kumuwezesha mdhibiti kutekeleza maamuzi yake, kuweka viwango vya ubora, kanuni na sera husika kwa maslahi ya umma.

Pia kuweka viwango katika maeneo sahihi yakiwemo ya kiufundi pamoja na huduma bora za kiumchumi.

ESAWAS ilianzishwa mwaka 2007 katika mkutano usio rasmi uliofanyika kati ya wadhibiti wa huduma za majisafi wa mazingira kutoka nchi tano za Afrika Mashariki na kusini waliopokutana kwaajili ya kubadilishana uzoefu na maarifa mbalimbali katika masuala yanayohusiana na maji na usafi wa mazingira.