TEA yaridhia ruzuku ya kujenga uzio Mlimani

BODI ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeridhia kutoa ufadhili wa ruzuku ya zaidi ya Sh milioni 496.6 kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa hosteli mpya za Mwalimu Julius Nyerere, Mlimani Kampasi.

Akizungumza wakati wa kusaini mkataba wa utekelezaji kati ya TEA na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kaimu Mkurugezi wa TEA, Graceana Shirima, alisema ujenzi wa uzio huo ni katika kuhakikishia usalama kwa wanafunzi watakaotumia hosteli hizo.

“TEA tumeamua kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za ujenzi wa hosteli kwa kujenga uzio katika hosteli ili kuweka usalama na ulinzi kwa wanachuo. Na hili tunalifanya kutokana na kuwa TEA kutekeleza miradi ya ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi wa kike na huu miradi ni wa hosteli ambazo zitachukua pia wanafunzi,” alisema Shirima.

Katika makubaliano hayo ya utekelezaji, uzio huo utajengwa ndani ya miezi 12 kuanzia sasa.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema ujenzi wa uzio huo unaojengwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tayari umeanza na kuahidi kuukamilisha ndani ya muda kama makubaliano yanavyotaka.

“Tayari ujenzi wa uzio umeanza kwa kuchimba msingi na unajengwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi, na kama mambo yatakwenda vizuri basi utakamilika ndani ya miezi mitatu na unaweza kuzinduliwa kabla hata ya mabweni,” alisema.

Pamoja na kuwashukuru TEA, Profesa Mukandala alisema ujenzi wa uzio huo utaondoa hali ya mwingiliano kati ya wanafunzi na jamii hivyo kuwaongezea usalama zaidi.

“Zile hoteli ziko karibu na eneo la kibiashara la Mlimani City, kituo cha mabasi, na pia kuna watu wengi wanapita, sasa ili kuwafanya wanafunzi kuwa salama tukaona tuweke uzio na tumefanya hivyo kwenye hosteli za Mabibo. “Pia kuna wazazi ambao wanawasiwasi na usalama wa mabweni hayo ambayo yanawezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 4,000, na tukifanya hivyo tutaimarisha ulinzi,” alisema Profesa Mukandala.

Alisema pia katika hosteli hizo, chuo kitajenga kituo cha polisi, kituo cha afya na kutakuwepo na gari la wagonjwa.