Washauriwa kujipanga kubadili sheria ya ndoa ya 1971

WABUNGE wametakiwa kuwa na mkakati wa pamoja ili mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 yafikishwe kwenye Bunge na kujadiliwa na wabunge ili sheria hiyo ipitishwe kwa maslahi ya ustawi wa watoto wa kike nchini.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa mtandao wa kupinga ndoa za utotoni uliowashirikisha wabunge. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema katika mkutano huo kuwa ushirikiano wa wabunge utasababisha mabadiliko ya sheria hiyo.

Waziri huyo alisema wabunge wanatakiwa kuwa na ushirikiano na sauti moja ili kuhakikisha marekebisho ya sheria hiyo yanafikishwa bungeni na kujadiliwa na hakuna sababu za ‘white paper’.

Mbunge wa Malindi, Ally Salehe (CUF) alisema kwa Zanzibar asilimia 24 ya watoto wa kike na asilimia sita ya watoto wa kiume wako kwenye ndoa.

“Tatizo ni kubwa sana watu wa mtandao ni lazima waoneshe ukubwa wa tatizo, dhana ya kuona wanaume ndio wanasababisha tatizo hilo halina mantiki yoyote kwani si kila mwanamume anafanya hivyo,” alisema.

Alisema kuna haja kama Bunge kuleta mabadiliko ya sheria ndani ya Bunge ili yajadiliwe na wabunge waache siasa ili kupitisha sheria hiyo. Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa (CCM) alisema ndoa za utotoni zimekithiri na zinaathiri afya za watoto wa kike na kusababisha vifo vya wasichana wadogo hususan nchi zinazoendelea.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM) alisema kwa muda mrefu kumekuwa na mapambano ya sheria kandamizi.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Tawfiq (CCM) alisema kuna haja kwa wabunge kwenda pamoja ili kuhakikisha sheria hiyo inafanyiwa marejebisho.

“Tukisimama kwa pamoja tutafanikisha jambo hili,” alisema Tawfiq.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema) alisema, “Tusipowatetea hao watoto tutawapoteza, jukumu la wabunge ni kuungana ili sheria ifanyiwe mabadiliko.

“Watoto wa kike wanakatisha masomo kwani anapoanza darasa la kwanza wanakuwa wengi wakienda sekondari wanapungua huko vyuo vikuu wanapungua kabisa,” alisema Lyimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Valerie Msoka, alisema Mkoa wa Shinyanga unaongozwa kwa kuwa na asilimia 59 ya ndoa za utotoni. Pia takwimu zinaonesha hapa nchini kila wanawake 100 wanawake 37 waliolewa chini ya miaka 18.