Simiyu yapata msukumo mkubwa kuendesha Jukwaa la Biashara

MBUNGE wa Itilima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, Njalu Silanga amesifu kuwapo kwa jukwaa la biashara la mkoa huo ambalo watendaji muhimu wa taasisi mbalimbali za kifedha na mamlaka ya mapato walikuwapo kuangalia fursa mbalimbali.

Jukwaa la Biashara Simiyu limeandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), wachapishaji wa magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Baadhi ya maofisa hao ambao taasisi zao ni wadau waliofanikisha Jukwaa hilo ni Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa NMB, Msoro Ngozi, Meneja wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo na Mkurugenzi Mkuu wa TIB, Frank Budege.

Pia kulikuwa na wawakilishi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Ofisa Mipango wa Meatu, Gervas Amata, aliliambia gazeti hili kwamba anashukuru sana kwa kitu alichoita dozi aliyoipata kwenye jukwaa hilo na kusema hana mashaka kwamba itachangia kuunyanyua mkoa huo mpya na wenye rasilimali nyingi na wenye kiu ya mabadiliko.

Akitoa nasaha katika jukwaa hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel alisema kutokana na ubunifu unaoendelea, Mkoa wa Simiyu hauonekani tena kama mkoa wa pembezoni na hivyo akawataka wananchi kuendelea kuwa wabunifu.

“Kwa mfano, hii miwani nimeinunua kwa ajili ya macho yangu kwani inanisaidia kuona vyema, lakini ikatokea macho yangu yakaona bila msaada wa miwani basi miwani hii haina thamani tena kwangu,” alisema Profesa Ole Gabriel.

Alisema mambo mengine muhimu ya kuzingatia katika biashara ni kuthamini wateja, kuepuka urasimu, kushughulikia changamoto kwa kuzigeuza kuwa fursa na kila jambo kulifikiria kimkakati.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema anamshukuru Rais John Magufuli kumpeleka kwenye mkoa wenye fursa nyingi na kwamba amedhamiria kwa dhati kutumia fursa hizo kuubadili mkoa huo kiuchumi na kuwa miongoni mwa mikoa yenye uchumi mkubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na kadhalika.

Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi aliwataka wafanyabiashara wa Simiyu kutumia Tekonolojia ya Mawasiliano ya Habari (Tehama) katika kufanya kazi zao kwani inarahisisha mambo mengi.

Dk Yonazi alisema mawasiliano baina yake na mkuu wa mkoa pamoja na wadau wengine waliofanikisha jukwaa hilo la biashara mkoani Simiyu jana yalifanyika kwa njia ya Tehama kwa maana ya kuwasiliana kwa ujumbe wa maandishi au WhatsApp.