Wahujumu wa uchumi kufilisiwa

MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga amefunguka na kusema kuwa watu wahaohujumu uchumi kwa kufanya biashara haramu, ikiwemo ya meno ya tembo watafilisiwa mali zao ili familia zao na jamii wajifunze kuhusu adhabu hiyo.

Amesema kamwe haitaweza kuacha watu wachache wanufaike na mali za uhalifu na hata kama ni wanafamilia watafungwa na mali zao zitafilisiwa.

Mganga aliyasema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hukumu iliyotolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyowahusisha wanandoa Peter Kabi na Leonida Kabi ambao wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.

Alisema hawawezi kukubali familia zinazohujumu uchumi kwani wanaharibu uchumi wa nchi na kwamba ni lazima wafilisiwe.

“Katika kesi hiyo ya wanafamilia tunakusudia kupeleka maombi maalumu ya kuwafilisi mali zao ikiwemo nyumba ambapo kulihifadhiwa meno ya tembo ili watoto wao na hata ndugu wengine waone uchungu wa kukaa kwenye nyumba ambayo si halali,” alisema DPP Mganga.

Alifafanua kuwa tayari mkoani Morogoro wamefilisi gari lenye namba za DFP ambalo limetumika kusafirisha biashara haramu huku mkoani Tanga wamefilisi magari mawili ambayo yalikuwa yametumika kusafirisha wahamiaji haramu kutoka Somalia.