Spika Bunge la Afrika Mashariki amfagilia Magufuli

SPIKA wa Bunge la Afrika Mashariki, Daniel Kidega amempongeza Rais John Magufuli kwa kazi kubwa ya kujenga uchumi wa Tanzania na amewaomba wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki kuunga mkono mfano mzuri unaooneshwa na kiongozi huyo.

Kidega alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na Dk Magufuli na kufanya naye mazungumzo yaliyojikita kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi wanachama, kuinua hali ya uchumi na kutatua matatizo yanayozikabili baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya.

“Nikueleze kitu kimoja, Tanzania na Afrika Mashariki tumebahatika sana kupata kiongozi kama Rais Magufuli ambaye anatuongoza vizuri, analeta maendeleo na mabadiliko,” alisisitiza Kidega.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke ambapo viongozi hao wamezungumzia namna Tanzania na Uingereza zitakavyoimarisha uhusiano na ushirikiano katika uwekezaji na biashara, mapambano dhidi ya Rushwa na dawa za kulevya, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuimarisha huduma za usafiri wa anga.

Dk Magufuli amemshukuru Balozi Cooke na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na uhusiano wake wa kihistoria na Uingereza katika kujenga uchumi imara wa Tanzania.

Aidha, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi Mpya wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Bhaswar Mukhopadhyay ambapo viongozi hao wamezungumzia juu ya shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa kwa ushirikiano wa Tanzania na IMF.

Mukhopadhyay alimpongeza Rais Magufuli kwa hatua kubwa na muhimu anazochukua kuimarisha uchumi.

Mbali na hao, jana Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Balozi Liberat Mfumukeko.