Wanachama 1,520 wa CCM watimuliwa kwa usaliti

WANACHAMA na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka ngazi ya shina, tawi, wilaya na mkoa wapatao 1,520 wamefukuzwa uanachama kwa makosa ya kukisaliti chama kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Taarifa iliyolifikia gazeti hili juzi ilieleza kuwa miongoni mwa waliofukuzwa ni pamoja na viongozi wa ngazi za wilaya, mkoa na taifa ambao ni tisa akiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC) Wilaya ya kichama ya Meru, Julius Mungure, na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Dk Wilfred Soilel.

Akizungumza jana jijini hapa na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Omari Billaly, alisema uamuzi ya NEC Mkoa iliyokutana Februari 11 mwaka huu kuhusu waliokisaliti chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.

Billaly alisema Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Arusha imetimiza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Ibara ya 93 (14).

Alisema halmashauri hiyo imeamua kuwafukuza uanachama wanachama hao baada ya kupatikana na makosa ya kukisaliti chama kwenye uchaguzi huo mkuu wa madiwani, wabunge na rais.

Alisema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi na maadili za CCM toleo la 2012 fungu la nane ibara ya 8(IX)(a) inajieleza wazi kuwa kosa kubwa kuliko yote katika CCM ni kukisaliti chama na kukiweka katika hali ya kushindwa katika uchaguzi wa dola.

Alisema lengo la chama cha siasa ni kushika dola kwa hiyo kiongozi au mwanachama yeyote anayethibitika kukisaliti chama adhabu yake kwa mujibu wa kanuni hizi ni kufukuzwa uanachama.

Wengine waliofukuzwa ambao ni viongozi ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Karatu na diwani wa Viti Maalum, Bibiana Nanyaro, na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, William Sarakikya.

Wengine ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM, Meru Aziza Mundo, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa Wilaya ya Arumeru Evaline Nanjway na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wazazi Wilaya ya Arumeru, Salome Samwel.

Aidha Kaimu Katibu huyo alitaja wilaya kwa idadi ya wanachama waliofukuzwa uanachama kwenye mabano kuwa ni Wilaya ya Meru (769), Ngorongoro (254), Monduli (202), Arusha( 172), Longido (64), Arumeru (58) na Wilaya ya Karatu mwanachama mmoja.

Pia halmashauri hiyo imetoa onyo kwa viongozi wa kamati ya siasa ya wilaya ya Karatu kwa kushindwa kusimamia jukumu la kuwabaini wasaliti na kwa kamati za siasa za kata zote mkoani Arusha ambazo hazikuwajadili waliokisaliti chama na wakati ccm ikishindwa katika uchaguzi wa udiwani kwenye kata tajwa.

Majina ya wilaya na idadi ya kata kwenye mabano ni Arumeru (9), Karatu (6), Longido (12), Arusha (2), Ngorongoro (4) na Monduli (3).

Kata katika wilaya ya Karatu zimepewa mwezi kukamilisha kuwabaini waliokisaliti chama kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Iwapo viongozi hawa waliofukuzwa uanachama hawakuridhika na adhabu hii ya kuwafukuza uanachama wanaweza kukata rufaa kwa Kamati Kuu (CC) ya CCM na ofisi ya Mkoa ipo wazi kuwasaidia ili kuhakikisha rufaa zao zinafikishwa kwa Katibu Mkuu wa CCM,” alisema.