Idara ya KAMILI UK.3 Uhamiaji kumfikisha Manji kortini

IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam imetangaza kumchukulia hatua ikiwemo kumfikisha mahakamani mfanyabiashara Yusuf Manji, akidaiwa kuajiri wafanyakazi wasio na vibali vya kuishi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Msumule alisema walifanya upekuzi mwishoni mwa wiki katika Kampuni ya Quality Group Limited (QGL) na kupata hati za kusafiria 126.

“Tulifanya kazi Ijumaa na Jumamosi saa kumi, tulipata pasipoti 126 na 25 hawana vibali vya kufanya kazi, hivyo wanafanya kazi kinyume na utaratibu,” alisema Msumule.

Alisema wote watafikishwa mahakamani na hawatapelekwa peke yao, bali watampeleka na Manji ambaye ndiye mwajiri wa watu hao na mmiliki wa kampuni hiyo kwa tuhuma za kuajiri watu wasio na vibali.

“Ilikuwa tumkamate na kumpeleka mahakamani bahati mbaya akawa amelazwa... mara atakapotoka atatakiwa kuwasili Uhamiaji tumuunganishe na kesi hii ya kuajiri watu wasio na vibali,” alieleza ofisa huyo akimzungumzia Manji, ambaye amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Manji alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa QGL hadi Julai mwaka jana, alipojiuzulu na kubaki kuwa Mshauri wa kampuni hiyo. Aliongeza, “hatutojali fedha, cheo chochote... utakamatwa, utawekwa ndani, utajibu mashitaka.

” Katika hatua nyingine, Msumule alisema wamekamata vibali feki vipatavyo vinane vya raia wa China huku wakiendelea na uchunguzi.

Aliwataja raia hao kuwa ni Hui Miao, Juntao Lu, Dongling Zhang, Caiholi Li, Anping Tang, Lijun Zhou na Ligang Who wote wa Kampuni ya Global Leader na Hui Cao wa Kampuni ya Herocean.

Aidha, alisema wamemkamata raia wa Uganda, Aisha Talib akiwa na hati za kusafiria 15 za raia wa mataifa mbalimbali.

Wakati huo huo, kati ya huduma za upasuaji za tiba na vipimo vya moyo zilizofanywa jana katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga na mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji ni miongoni mwa wagonjwa waliopewa huduma.

Mwandishi wetu alimshuhudia Manji akiwa amelala kwenye kitanda cha wagonjwa, akisukumwa na wahudumu wa hospitali hiyo akitokea chumba cha upasuaji.

Taasisi hiyo juzi na jana ilifanya tiba pamoja na uchunguzi wa moyo kwa wagonjwa 20 chini ya usimamizi wa daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka India, Dk Subhash Chandra.

Mbali na wahudumu wa hospitali, kitanda cha Manji pia kilizungukwa na wanaume wengine wawili, ambao walikuwa na nguo za kawaida pamoja na askari aliyekuwa amevaa sare za Jeshi la Polisi.

Baada ya kutolewa kwenye chumba cha upasuaji, Manji aliyekuwa amelala kwenye kitanda hicho, alionekana mara kadhaa akijaribu kufumbua macho na kuinua kichwa huku akiwa amekunja uso kuonesha kuwa alikuwa na maumivu na kukirudisha chini.

Hata hivyo, kitanda chake kilisukumwa na kuingizwa ndani ya lifti na baadaye kuondoka kuelekea juu kwenye wodi za wagonjwa.

Msemaji wa taasisi hiyo, Anna Nkinda alipoulizwa ni tatizo gani la moyo alilonalo Manji, alisema tatizo la mgonjwa ni siri yake mwenyewe na hawaruhusiwi kutoa taarifa hizo.

“Ni kweli Manji yuko hapa, lakini kuhusu tatizo lake hilo hatuwezi kusema kwa sababu ni siri ya mgonjwa mwenyewe, na kuhusu lini tulimpokea hapa pia hatutatoa taarifa hizo,” alieleza Nkinda.

Siku tatu zilizopita mfanyabiashara hiyo aliyekuwa ameshikiliwa na Jeshi la Polisi Kituo Kikuu jijini Dar es Salaam kwa mahojiano kuhusu suala la dawa za kulevya, alionekana akipandishwa katika gari la wagonjwa na kuondolewa kituoni hapo.

Manji ni miongoni mwa majina yaliyotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhusu dawa za kulevya, na aliwasili kituo hicho cha polisi Alhamisi iliyopita kwa mahojiano, badala ya Ijumaa kama alivyotakiwa.

Hata hivyo, baada ya kuwasili kituoni hapo, aliendelea kushikiliwa na jeshi hilo mpaka siku ambayo alionekana anaondolewa na gari la wagonjwa.