Malori ya makontena yabakiza wiki 9 Dar

BANDARI Kavu (ICD) ya Ruvu mkoani Pwani, ambayo ujenzi wake unalenga kupunguza msongamano wa malori jijini Dar es Salaam, utakamilika ndani ya wiki tisa zijazo na utagharimu Sh bilioni 7.3.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba ujenzi huo unafanywa na Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT), ambao jana walisaini mkataba wa ujenzi huo na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Profesa Mbarawa alisema mara tu ujenzi huo utakapokamilika, makontena yote yatapelekwa kwenye bandari hiyo ya Ruvu kwa reli na malori yanayotoka mikoani na nchi jirani, yatakuwa yanachukulia mizigo yao huko badala ya kuja Dar es Salaam.

“Tunatarajia kuwa ujenzi ukikamilika ndani ya wiki hizo tisa, bandari hiyo itaanza kufanya kazi,” alifafanua Profesa Mbarawa.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo, kutaleta ufanisi mkubwa katika bandari ya Dar es Salaam, kwa kuwa hakutakuwa tena na msongamano wa makontena.

Alisema ni mpango wa serikali kwamba bandaria kavu zote za jijini Dar es Salaam, zijengwe nje ya mji ili kupunguza msongamano wa magari.

Alisema kujengwa kwa Ruvu ICD, kutasaidia kupunguza msongamano wa magari, kwani malori yote ambayo kwa sasa yanalazimika kufika bandarini kwa ajili ya kuchukua shehena mbalimbali yatakomea Ruvu.

Alisema serikali imeamua kuwapa Suma JKT kujenga bandari hiyo, kwa kuwa wanawaamini kwamba wataufanya ndani ya muda uliopangwa na kwa ufanisi mkubwa.

“Sisi hawa hatuwaangalii kama JKT, bali tunawaangalia kama wakandarasi, hivyo tutaendelea kumsimamia kuhakikisha anakamilisha kazi kwa muda tuliokubaliana,” alieleza.

Naye Mwanasheria wa Suma JKT, Kanali John Mbungo ambaye alisaini mkataba huo kwa niaba ya JKT, alisema TPA waendelee kuwaamini kwani wataifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.

Kanali Mbungo alisema Suma JKT wana uzoefu mkubwa wa kujenga miradi mbalimbali ya serikali kwa muda mfupi, zikiwemo nyumba za serikali zilizojengwa jijini Dar es Salaam na mkoani Dodoma.

Aidha, Profesa Mbarawa alisema kwamba licha ya mradi huo wa ICD Ruvu, mwezi ujao serikali itatia saini ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300 katika bandari ya Mtwara.

Alisema ujenzi wa gati hilo, utawezesha meli za ukubwa wowote kutia nanga, jambo ambalo litasaidia mizigo mikubwa kufikishwa kwenye bandari hiyo.

Pia alisema kwamba TPA itaipanua bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuongeza kina ili kuwezesha meli kubwa ambazo kwa sasa zinashindwa kutia nanga bandarini hapo kutokana na kina cha maji kubwa kifupi zifike.

Alisema juhudi hizo za serikali za kuboresha bandari zake zinalenga kuhakikisha kwamba wanawavutia wateja wengi ambao wanatumia bandari hiyo.

“Naamini kwamba tukikamilisha miradi yote hii, bandari yetu itakuwa na uwezo wa kushindana na bandari nyingine yoyote katika katika ukanda huu wa mashariki mwa Afrika,” alieleza waziri huyo wa sekta za ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.

Alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam Septemba mwaka jana, Rais John Magufuli aliitaka TPA kujipanga kujenga bandari kavu (ICD) Ruvu mkoani Pwani.

Aliitaka TPA iache kuzitegemea bandari kavu zilizoanzishwa na watu binafsi jijini Dar es Salaam kwa kuwa zinatumika kukwepa kodi.

Aidha, alipoweka jiwe la msingi la mradi wa barabara ya juu katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela, Rais Magufuli alisema reli ya kisasa itakapofika Ruvu, kutajengwa bandari kavu kubwa katika eneo hilo, ambayo ikikamilika mizigo yote inayoshuka Bandari ya Dar es Salaam, itasafirishwa kwa reli mpaka katika bandari hiyo.

Rais Magufuli alisema malori yote yanayochukua na kupeleka mizigo katika bandari hiyo, yataishia katika bandari kavu ya Ruvu na kupigwa marufuku kuonekana katika Jiji la Dar es Salaam.