Serikali yapongezwa kudhibiti ‘unga’

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, ameipongeza serikali kwa juhudi za kudhibiti dawa za kulevya na kusema kuwa, imeonesha dhahiri kutekeleza Ilani ya chama hicho.

Madabida alitoa pongezi hizo jijini humo juzi wakati wa mkutano ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuhusu kutangazwa kwa awamu ya tatu orodha ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Alisema mwaka 2015 CCM ilizunguka nchi nzima kuomba ridhaa ya wananchi kuwaongoza na walikwenda na ilani ya chama na jambo kubwa waliloliahidi ni mapambano dhidi ya dawa za kulevya ambazo zina madhara makubwa hususani kwa vijana.

Aliongeza kuwa, kupitia ilani hiyo ya chama kimeelekeza serikali kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kuanzisha mamlaka ya kudhibiti na kuzuia dawa za kulevya, kuongeza utoaji wa dawa kwa waathirika na vituo, kushirikiana na asasi za kijamii katika kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya pamoja na kusimamia kikamilifu sheria mpya ya kudhibiti dawa za kulevya.

“Mambo yanayofanywa na Rais John Magufuli na Mkuu wa Mkoa wetu si mambo ya kujitungia wao wenyewe yapo kwenye ilani, mimi nipo hapa kushuhudia kama kweli yale tuliyoyaagiza wanatekeleza na wasipotekeleza tutawawajibisha,” alisema Madabida.

Alisema jambo ambalo wanajivunia na limetekelezwa mpaka sasa ni kuanzishwa kwa mamlaka ya udhibiti na kuzuia dawa za kulevya pamoja na kusimamia kikamilifu sheria mpya ya dawa za kulevya.

“Ili haya yote yafanikiwe sisi sote tunahitaji kuwaunga mkono kwasababu watu wote wauzaji, wasambazaji, watumiaji wapo katika mazingira yetu tunaishi nao naomba nimpongeze rais kwa kusimama imara dhidi ya madhira haya, Mkuu wa Mkoa nakupongeza.

Kamishna mkuu kazi hii inataka ujasiri, kujitolea, uadilifu na uwezo wa kutenda haki.