Waandishi washuhudia uzibuaji wa valvu ya moyo JKCI

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imefanya matibabu ya moyo kwa wagonjwa 16 ndani ya siku mbili, ikiwa ni matibabu ya kuwafanyia upasuaji wa moyo bila kuwapasua vifua vyao.

Aidha, waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali walishuhudia upasuaji huo jana, ikiwa ni wa kuzibua valvu ya moyo ambayo mgonjwa alifanyiwa na kumaliza akiwa salama chini ya dakika 20.

Akizungumza na waandishi wa habari katika chumba cha upasuaji cha taasisi hiyo jana, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Dk Peter Kisenge alisema lengo la taasisi hiyo kwa siku hizo mbili ni kufanya upasuaji kwa wagonjwa 20.

Dk Kisenge alisema katika upasuaji huo walizibua valvu zilizoziba (sita), kuwawekea wagonjwa betri za moyo (watatu) na kuzibua mishipa ya moyo iliyoziba (watatu) na nyingine zikiwa za vipimo vya moyo.

Alisema kufanikiwa kwa upasuaji huo wa wagonjwa umeokoa fedha nyingi kwani mgonjwa mmoja kwenda kufanya upasuaji wa aina hiyo nje ya nchi ni zaidi ya Sh milioni 25.

Dk Kisenge alisema upasuaji huo ulifanyika, wakiongozwa na Dk Subhash Chandra Mwenyekiti wa Taasisi ya Moyo Vigyat Singh ya India.

“Hii ni mara ya pili kwetu kufanya aina hii ya upasuaji kwa wagonjwa kuwatanua valvu, lakini ni mara ya kwanza kwetu kwa valvu zilizoziba kupita kiasi, na wagonjwa wote tuliowafanyia wanaendelea vizuri hawakufanyiwa upasuaji wowote mkubwa, tumefanya bila kupasua,” alisema Dk Kisenge.

Mmoja ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kuzibua valvu za moyo, Fatma Mahenge alisema amepata huduma nzuri katika taasisi hiyo na kwamba anaamini amepona kabisa baada ya upasuaji huo.