Vita dawa za kulevya mbele kwa mbele

WAKATI Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisema serikali imeweka nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya, amewataka watendaji wote kuanzia ngazi ya vijiji wadhibiti suala hilo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema inaunga mkono mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

“Serikali haiwezi kuona vijana wanaangamia kwa dawa za kulevya. Tumeamua kudhibiti hali hiyo. Hii vita ni ya nchi nzima. Kuanzia sasa, viongozi wa serikali za vijiji wakamateni wale wote wanaojihusisha na biashara hii,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza: “Tunataka vijiji vyetu, kata zetu, wilaya zetu na mikoa yetu iwe safi bila hata chembe ya dawa za kulevya.

Tukikuona kijana unayumbayumba au kuweweseka, tunakupima na tukikuta umetumia ile kitu, tunakukamata ili utuambie ni nani amekupa. “Sisi tunataka vijana wafanye kazi za kujiletea maendeleo. Kijana hawezi kuwa na maendeleo wakati hufanyi kazi, huwezi kuwa na ndoto za maendeleo wakati umelewa bangi au dawa za kulevya. Kila mmoja afanye kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu”.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo jana katika Kijiji cha Engusero wilayani Kiteto baada ya kusimamishwa na wananchi wakati akiwa njiani kwenda mjini Kibaya yalipo makao makuu ya wilaya hiyo ili aanze ziara ya kikazi ya Mkoa wa Manyara. Wakati Majaliwa akisema hayo, SMZ imesema inaunga mkono mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kusema vyombo vya ulinzi vinatakiwa kusimamia utekelezaji wa agizo la Serikali Kuu kikamilifu.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, Ali Salum aliyetaka kufahamu mikakati ya kupambana na vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana ambavyo ndiyo vinavyochangia uhalifu.

Alisema makamanda wa Polisi wa Mkoa na wilaya, moja ya kipimo cha kazi zai ni kupambana na dawa za kulevya katika sehemu zao.

Alisema ni kweli tatizo la dawa za kulevya ni kubwa na athari zake zimejitokeza waziwazi kwa jamii ya vijana ambayo imeathirika kwa kujiingiza katika vitendo vinavyokiuka maadili ya taifa.

Alitoa mfano kuwa, baadhi ya matukio mbalimbali ya uhalifu yanafanywa na kundi la vijana wanaojihusisha na dawa ya kulevya ikiwemo uporaji.

Alisema katika kukabiliana na matukio hayo, serikali imewaagiza viongozi wa vyombo vya ulinzi kuhakikisha wanapambana na matukio hayo na kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kujishughulisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema katika juhudi za kupambana na dawa za kulevya, Zanzibar imeanzisha Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo miongoni mwa majukumu yake ulisimamia tatizo hilo kwa nguvu zote za kisheria.

Aidha, amewataka wananchi kutoa ushirikiano na taarifa za kuwepo kwa dawa ya kulevya au mtu anayejishughulisha na biashara hiyo ambayo hivi sasa viongozi wa kitaifa wametangaza kuwa ni vita vya mapambano.