Wakuu EAC watakiwa kulinda Ziwa Victoria

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhakikisha wanatunza na kuhifadhi bonde la Ziwa Victoria kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aliyasema hayo jana jijini hapa alipofungua kongamano la kisayansi la siku mbili lililohudhuriwa na wanasayansi na watafiti kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na wenyeji Tanzania.

Alisema Ziwa Victoria ni rasilimali muhimu kwa wananchi wa nchi za Afrika Mashariki kwa sababu ni chanzo cha ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo na ni chanzo kubwa cha maji kwa ajili ya matumizi ya watu kwa nchi hizo.

“Hivyo ni jukumu letu kuhakikisha kuwa ziwa hili linalohitajiwa na watu wengi duniani, linalindwa kwa kupitia njia zote za kisayansi kwa ajili yetu na vizazi vijavyo,” alieleza.

Hata hivyo, alisema ziwa hilo bado linakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo shughuli za kiuchumi zinazofanywa kuzunguka ziwa hilo, ikiwa ni pamoja na magugumaji yanayoathiri ubora wa maji, uvuvi na shughuli za usafirishaji.

Naye, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Dk Ally Matano alisema Ziwa Victoria linakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile uchafuzi unaotokana na shughuli za viwanda, shughuli za kiuchumi kando ya ziwa na gugumaji.

Alisema nchi wanachama zinazofanya kazi kupitia Bonde la Ziwa Victoria zimechukua hatua kadhaa katika kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuwa na sheria na sera za pamoja kwa nchi wanachama ambapo baadhi ya changamoto hizo zimeanza kushughulikiwa.

Aliongeza kuwa, mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili tafiti mbalimbali zilizofanywa na watalaamu ili kubadilishana uzoefu na namna bora ya kutunza ziwa hilo sambamba na kujadili changamoto zinazolikumba ziwa hilo.

Naibu Katibu Mkuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Christophe Bazivamo alisema nchi wanachama wa EAC zinakabiliana na changamoto nyingi za mazingira ambazo hurudisha nyuma juhudi za kuboresha maisha ya watu katika nchi hizo.