Vituo 155 vya QT kufutiwa usajili

TAASISI ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), inatarajia kuvifuta vituo 155 vinavyotoa mafunzo ya elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi maarufu kama QT kutokana na kukiuka taratibu zilizowekwa na kushindwa kufuata masharti ya usajili.

Naibu Mkurugenzi Taaluma wa taasisi hiyo, Dk Kassim Nihuka aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango wa utoaji elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi kwa njia ya mafunzo ya jioni.

Dk Nihuka alisema miongoni mwa masharti yaliyokiukwa na vituo hivyo ni kutokulipa ada ya uratibu ambayo ni Sh 20,000 kwa kila mwanafunzi aliyesajiliwa na vingine mazingira yake ya kufundishia hayaridhishi.

Alisema kutokana na hali hiyo, taasisi hiyo imetoa muda kwa waendeshaji wa vituo hivyo ili warekebishe kasoro hizo na ifikapo Machi mosi mwaka huu kama hawajazishughulikia changamoto zao, vituo hivyo vitafungiwa.

Dk Nihuka alisema mpaka sasa kuna vituo 420 nchi nzima vinavyotoa mafunzo ya elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi, na kati ya hivyo, vituo 337 ni vya wadau na 83 vinasimamiwa na TEWW.

Alisema kati ya hivyo, vituo 182 vimesajiliwa na vimefuata taratibu zinazotakiwa, lakini vituo 155 vimekiuka taratibu hivyo viko hatarini kufutwa kutokana na kukiuka taratibu zinazotakiwa.

“Programu hii ambayo inaendeshwa katika majengo ya shule za msingi na sekondari za serikali ni vituo 83 na shule za wadau mbalimbali 337 nchini zimewanufaisha vijana na watu wazima 95,140 tangu mwaka 2010 hadi 2016,” alieleza Naibu Mkurugenzi huyo.

Pia alisema kwa wanafunzi wanaosoma katika mfumo huo wenye miaka chini ya 23 wakimaliza elimu ya kidato cha nne na kufaulu vizuri ana fursa ya kuendelea na masomo kama wanafunzi wengine ya kidato cha tano na sita, lakini mwenye miaka zaidi ya 25 atasoma kwa mwaka mmoja kidato cha tano na sita.

Alisema katika programu hiyo masomo yanayotolewa katika hatua tatu kubwa moja ikiwa hatua ya kwanza inabeba masomo ya kidato cha kwanza na cha pili, hatua ya pili inabeba kidato cha tatu na nne na hatua ya tatu inabeba hatua ya kidato cha tano na sita.

Aidha, alisema mlengwa anasoma kwa mwaka mmoja na kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa maarifa na anasoma masomo saba ambayo yanatolewa katika hatua hiyo ambayo ni Historia, Jiografia, Kiingereza, Kiswahili, Hisabati, Biolojia na Uraia.